Manchester, England
Kocha wa muda wa Man United, Michael Carrick amesisitiza kuwa hasikilizi kauli zikiwamo za mchezaji mwenzake wa zamani wa timu hiyo, Wayne Rooney kudai kwamba kocha huyo sasa anatakiwa kupewa mkataba wa kudumu.
Ushindi wa mabao 3-1 ambao Man United iliupata Jumapili dhidi ya Aston Villa umezidi kumpaisha kocha huyo na hatimaye kuibua hoja ya kuwataka mabosi wa klabu kumpa mkataba wa kudumu.
Huo ni ushindi wa saba katika mechi tisa za Carrick, ushindi ambao umeianya timu hiyo kuiacha Chelsea inayoshika nafasi ya sita kwa tofauti ya pointi sita na kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Matokeo hayo yamemfanya Rooney katika mazungumzo yake na kituo kimoja cha redio kusema kwamba sasa ni kwa asilimia 100, Carrick anatakiwa kupewa mkataba wa kudumu Man United.
Rooney alifafanua kuwa anamjua vizuri Carrick na tabia zake na jinsi alivyo katika timu ambayo inahitaji mtu mwenye utulivu na ambaye anaijua timu hiyo na wachezaji ambao wanahitaji upendo na anawapa vyote hivyo.
Kwa upande wake Carrick alipoulizwa kuhusu hilo alicheka na kupuuza kila kinachozungumzwa na kusema kwamba hizo ni kelele tu za jumla na si Rooney pekee yake.
“Hazina madhara yoyote kwangu, kwa wakati huu nipo katika kazi ambayo naifanya kwa ubora wangu na tunaendelea kupambana zaidi na zaidi, tunataka kuifanya timu iwe bora kadri iwezekanavyo, lolote linaloweza kutokea tuache litokee,” alisema.
Nahodha wa timu hiyo, Bruno Fernandes ameendelea kuwa mtu muhimu kikosini akitoa pasi muhimu zinazozaa mabao, katika mechi na Villa alitoa pasi mbili ambazo Cunha na Casemiro walizitumia kuipatia Man United mabao.
