Tunis, Tunisia
Kocha mkuu wa timu ya Esperance ya Tunisia, Patrice Beaumelle amesema timu yake itawakabili kwa nguvu zote Al Ahly katika mechi ya kwanza ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Jumapili Machi 15, 2026.
Esperance waliokuwa kundi D na timu za Simba ya Tanzania, Stade Malien ya Mali na Petro Atletico ya Angola walifuzu kucheza robo fainali ya michuano hiyo ingawa mwenendo wa timu haukuwa mzuri.
Kutokana na mwenendo wa timu kutokuwa mzuri, Maher Kanzari alitimuliwa na nafasi yake kupewa Beaumelle ambaye mtihani wake wa kwanza mkubwa utakuwa dhidi ya Ahly.
Katika Kundi D, mbali na Esperance, timu nyingine iliyofuzu robo fainali ni Stade Malien ambayo tayari imeanza vibaya mechi ya kwanza ya hatua hiyo kwa kulala kwa mabao 3-0 mbele ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Esperance itakuwa mwenyeji katika mechi ya kwanza na Ahly katika dimba la Hammadi Agrebi kabla ya timu hizo kurudiana Jumamosi ijayo mjini Cairo.
Beaumelle alisisitiza Esperance lazima itumie fursa ya kuwa mwenyeji wa mechi ya kwanza mbele ya mashabiki wake na matumaini yake ni kwamba mechi hiyo inaweza kuwapa faida wakati timu hizo zitakapokutana mara ya pili mjini Cairo.
“Tuna mechi ya nyumbani na ni lzima tucheze kwa nguvu zetu zote, katika mechi ya kwanza tunatakiwa kujitoa kwa kila kitu mbele ya mashabiki wetu ili tuweze kuwa na nafasi ya kucheza katika namna bora kadri iwezekanavyo katika mechi ya marudiano,” alisema Beaumelle.
Esperance itacheza mechi na Ahly ikiwa imetoka kurekodi ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tunisia dhidi ya Future Marsa.
Katika mechi hiyo, Beaumelle alifanya mabadiliko ya haraka haraka kwa baadhi ya wachezaji muhimu kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutotaka kuumiza wachezaji wake kabla ya mechi dhidi ya Ahly.
