London, England
Mshambuliaji wa zamani wa Tottenham Hotspur, Jurgen Klinsmann (pichani) amekataa kujiweka kando na uwezekano wa kuwa kocha wa timu hiyo wakati huu kocha wa sasa, Igor Tudor akipitia kipindi kigumu.
Tudor amekuwa kocha wa Spurs tangu mwezi uliopita lakini matokeo mabaya ya kufungwa mechi nne mfululizo yaliyoiacha timu hiyo ikipambana na janga la kushuka daraja yanaweza kumfanya atimuliwe kama alivyokuwa mtangulizi wake, Thomas Frank.
Mechi tisa zilizobaki za Ligi Kuu England ndizo zitakazoamua kama Spurs itabaki katika ligi hiyo kubwa barani Ulaya au itashuka, mazingira ambayo yanatoa picha kwamba nafasi ya kocha wa timu hiyo ipo njia panda.
Klinsmann ambaye enzi zake za kucheza soka la ushindani pia alikuwa akiichezea timu ya taifa ya Ujerumani, bado hajafanya mazungumzo yoyote na mabosi wa Spurs ingawa kwa sasa jina la Sean Dyche nalo limekuwa likitajwa.
Akiwa Spurs enzi zake, Klinsmann aliichezea timu hiyo mechi 68 na kufunga mabao 37, alipoulizwa kuhusu kuinoa timu hiyo alisema kwamba hakuna anayekataa kazi hiyo.
“Nani atakayeikataa kazi hiyo, yeyote utakayemchagua utahitaji mtu atakayekuwa kiunganishi kwa kila hali, mtu anayeijua klabu, ana mtazamo wa klabu na mwenye fikra za watu,” alisema Klinsmann.
Alisema kwamba kwa vyovyote itakavyokuwa ili kuondoka katika hali mbaya waliyopo ni lazima kujenga hali ya upambanaji wa nguvu na hilo ni lazima liwe katika fikra za watu.
Katika mazingira kama hayo, Klinsmann anaamini si suala la kuanza kutengeneza mbinu tu na yanayohusiana na hayo badala yake kila mtu kuingia vitani kupambana na kuwa katika msimamo chanya kukimbia uwezekano wa kushuka daraja.
