Rabat, Morocco
Baada ya kuiongoza kwa mafanikio timu ya taifa ya Morocco, kocha Walid Regragui (pichani) ametangaza kuachana na timu hiyo maarufu Atlas Lion na tayari Mohamed Ouah ameteuliwa kushika nafasi hiyo.
Uamuzi wa kocha huyo uliotangazwa moja kwa moja kupitia televisheni, umekuja ikiwa imebaki takriban miezi mitatu kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia 2026.
Katika kipindi cha miaka mitatu na nusu cha kuiongoza timu hiyo, Regragui amewahi kutwaa tuzo ya kocha bora wa mwaka wa CAF kwa mwaka 2022 ikiwa ni tuzo ya kwanza kwa kocha kutoka Morocco.
Baada ya kukabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo Agosti, 2022, Regragui aliiongoza vyema timu hiyo hadi kuiwezesha kufikia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022 katika fainali zilizofanyika, Qatar.
Mafanikio hayo yalimfanya Regragui kuweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kuiongoza timu ya Afrika kufikia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia katika historia ya michuano hiyo.
Katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zilizofanyika hivi karibuni nchini Morocco, kocha huyo aliiongoza Morocco kufikia hatua ya fainali ya michuano hiyo.
“Naacha majukumu kwa uadilifu, heshima na uhakika kwamba nimeisaidia nchi yangu, timu inahitaji sura mpya, nguvu tofauti, mtazamo mpya ikiwa na kocha mpya kabla ya Kombe la Dunia ili kuendeleza mafanikio, uamuzi wangu wa kuachana na timu hii ni wa kuendelea kuibadili na kuipa mafanikio,” alisema Regragui.
Baada ya Regragui kuachia ngazi, Shirikisho la Soka Morocco limemteua Mohamed Ouah kuchukua nafasi hiyo kazi ambayo anaianza mara moja.
Uteuzi wa Ouahbi umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mafanikio aliyoyapata akiwa na timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Morocco ambayo Oktoba mwaka jana ilifanya vizuri kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa vijana nchini Chile.
