Tunis, Tunia
Kocha Patrice Beaumelle (pichani) mwenye asili ya Ufaransa ameteuliwa kuwa kocha mkuu mpya wa klabu ya Esperance ya Tunisia na amesaini mkataba utakaomfanya awe na timu hiyo hadi Juni, 2027.
Beaumelle, 47, amekabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo akichukua nafasi ya Maher Kanzari ambaye alifutwa kazi mapema mwezi huu baada ya timu hiyo kuwa na matokeo yasiyoridhisha.
Miongoni mwa matokeo hayo ni kipigo cha bao 1-0 ambacho Esperance ilikipata kwa Stade Malien katika mechi ya mwisho hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ingawa timu hiyo imefuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Mtihani wa kwanza mkubwa kwa kocha huyo ambaye amejiunga na timu hiyo na jopo la wasaidizi wake, utakuwa wiki ijayo ambapo Esperance itaumana na vigogo Al Ahly ya Misri katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Beaumelle ametua Esperance baada ya kuvunja mkataba wake na Shirikisho la Soka Angola alipokuwa akiinoa timu ya taifa ya nchi hiyo ambayo alikuwa nayo kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka jana mwishoni nchini Morocco.
Kocha huyo si mgeni katika soka la Afrika, aliwahi kuwa mmoja wa wasaidizi wa kocha Mfaransa, Hervé Renard ambaye mwaka 2012 aliiongoza timu ya taifa ya Zambia maarufu Chipolopolo hadi kubeba taji la Afcon na wakawa tena pamoja mwaka 2015 na timu ya Ivory Coast iliyobeba taji hilo.
Kwa upande wa klabu, Beaumelle amejipatia mafanikio zaidi nchini Algeria wakati akiinoa Mouloudia Club d’Alger, timu aliyoiwezesha kubeba taji la Ligi Kuu Algeria msimu wa 2023-24 na kufika hatua ya fainali Kombe la Algeria msimu huo huo.
Kimataifa Kocha Mfaransa akabidhiwa Esperance
Kocha Mfaransa akabidhiwa Esperance
Read also
