Rabat, Morocco
Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Morocco, Romain Saiss (pichani) ametangaza kujiuzulu kuichezea timu ya taifa akiwa na umri wa miaka 34, baada ya kuichezea timu hiyo kwa zaidi ya miaka 10.
Saiss, beki kisiki wa kati aliyejipatia umaarufu alitangaza uamuzi huo hivi karibuni kupitia mitandao ya kijuamii akielezea kuwa wakati wake kwenye timu ya taifa ya Morocco au Atlas Lion ulikuwa mzuri katika maisha yake ya soka.
Katika kipindi chote ambacho amekuwa na timu hiyo, Saiss amecheza jumla ya mechi 86 na kuwa nahodha wa timu hiyo katika kipindi cha mafanikio zaidi katika historia ya soka nchini Morocco.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kufikia hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 na kuweka rekodi ya kihistoria kwa kuwa timu ya kwanza kutoka bara la Afrika kufikia hatua hiyo.
“Leo nakamilisha ukurasa mzuri zaidi katika maisha yangu ya soka, baada ya kutafakari kwa kina, natangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa nikiwa mwenye hamasa kubwa, kuivaa jezi ya timu ya taifa ya Morocco na kuongoza timu hiyo inabaki kuwa heshima kubwa katika maisha yangu ya soka,” alisema Saiss.
Kwa kipindi chote ambacho amekuwa na timu ya taifa ya Morocco, Saiss amejijengea heshima akiwa mmoja wa mabeki imara wa kati wa timu hiyo na kiongozi aliyeheshimiwa na wachezaji wenzake.
