Benfica, Ureno
Klabu ya Benfica ya Ureno imewasimamisha mashabiki wake watano baada ya uchunguzi kubaini walijihusisha na vitendo vyenye viashiria vya ubaguzi wa rangi katika mechi yao dhidi ya Real Madrid hivi karibuni.
Taarifa ya klabu hiyo ilieleza kuwa imechukua hatua hizo za kinidhamu dhidi ya mashabiki wake ambao huenda baadaye hatua zaidi zikachukuliwa ikiwamo uwezekano wa mashabiki hao kufungiwa.
Katika mechi hiyo ambayo ni ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baadhi ya mashabiki wa Benfica wakiwa uwanja wao wa nyumbani walitoa dhihara ya ishara za nyani ambazo mara nyingi hufanyiwa wachezaji weusi au wenye asili ya Afrika.
Mashabiki hao ambao pia ni wanachama wa klabu hiyo wamesimamishwa uanachama baada ya kikao cha kamati ya nidhamu ambapo baadaye hatua zaidi zinatarajia kuchukuliwa kwa mujibu wa kanuni za klabu hiyo.
“Uchunguzi wa ndani uliofanywa baada ya mechi kati ya Benfica na Real Madrid iliyochezwa Februari 17 umebaini kuwapo vitendo visivyokubalika vyenye viashiria vya ubaguzi wa rangi katika majukwaa, vitendo ambavyo haviendani na miiko ya klabu,” ilieleza taarifa ya Benfica.
Benfica katika taarifa hiyo pia waliuhakikishia umma kuwa klabu yao haivumilii aina yoyote ya ubaguzi ikiwamo ubaguzi wa rangi na wataendelea kuchukua hatua kali dhidi ya tabia zozote zinazoshusha hadhi ya klabu hiyo.
Mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kati ya timu hizo ilisimamishwa kwa dakika kadhaa mwamuzi alipoamua kutumia kanuni za kupinga ubaguzi wa rangi kwenye soka baada ya kuwapo tuhuma kwamba nyota wa Real Madrid, Vinicius Juior alifanyiwa dhihaka za kibaguzi na mshambuliaji wa Benfica, Gianluca Prestianni.
Prestianni, nyota kutoka Argentina hata hivyo alikana tuhuma hizo na hata klabu yake ilimtetea ikidai kuwa kilichopo ni sehemu ya mkakati wa kumuingiza mchezaji wao katika kesi ya udhililishaji.
