Riyadh, Saudi Arabia
Cristiano Ronaldo ametupia kambani katika ushindi wa mabao 5-0 ambao Al Nassr iliupata jana Jumatano Februari 25, 2026 dhidi ya Al Najma na kuiwezesha timu hiyo kushika usukani kwenye msimamo wa ligi.
Hilo ni bao la tatu kwa Ronaldo tangu asitishe mgomo baridi na kuanza kuitumikia timu hiyo inayopambana katika mechi za Ligi Kuu Saudi Arabia maarufu Saudi Pro League.
Ronaldo ndiye aliyeanza kufungua ukurasa wa mabao baada ya kufunga kwa mkwaju wa penalti mapema dakika ya saba ya mchezo na hivyo kumfanya afikishe mabao 20 msimu huu akiwa amezidiwa katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu na Ivan Toney wa Al Ahli mwenye mabao 23.
Kasi ya Al Nassr iliendelea na kuzaa mabao mawili yaliyofungwa na Kingsley Coman na Inigo Martinez, mabao ambayo yalizifanya timu hizo ziende mapumziko Al Nassr wakiwa mbele kwa mabao 3-0.
Mabao mengine ya Al Nassr yalipachikwa wavuni na Sadio Mane mapema katika kipindi cha pili wakati ambao kocha wa timu hiyo, Jorge Jesus alianza kufanya mabadiliko kwa kuwatoa baadhi ya mastaa akiwamo Ronaldo.
Al Nassr inashika usukani wa ligi hiyo ikiwa imefikisha pointi 58 katika mechi 23 na hadi sasa imepoteza mechi moja tu na imewazidi kwa pointi mbili, Al Ahli wanaoshika nafasi ya pili.
Mapema mwezi huu Ronaldo alikosa mechi mbili za timu yake dhidi ya Al Ittihad na Al Riyadh kutokana na kilichodaiwa kuwa ni mgomo baridi aliouanzisha akipinga masuala kadhaa ya uendeshaji wa klabu na ligi ya Saudi Arabia.
Kimataifa Ronaldo apiga bao, Al Nassr kileleni
Ronaldo apiga bao, Al Nassr kileleni
Read also
