Miami, Marekani
Mshambuliaji wa timu ya Inter Miami ya Marekani, Lionel Messi amesema kwamba kati ya mambo anayojutia akiwa mdogo ni kitendo cha kutojifunza lugha ya kingereza katika masomo yake wakati huo.
Messi, 38, ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, amesema kuna wakati alijiona kama mjinga hasa alipokutana na watu maarufu wakati akifurahia mafanikio katika maisha yake ya soka lakini hakuweza kuzungumza nao.
“Kuna mambo mengi ninayojuta, moja ni kutojifunza lugha ya Kiingereza wakati nikiwa kijana mdogo, nilikuwa na fursa ya kujifunza Kiingereza lakini sikufanya hivyo, najuta sana kwa hilo,” alisema Messi.
Messi alisema kwamba kuna wakati alikuwa katika mazingira ambayo alikutana na watu maarufu na wenye sifa za kipekee na ambao angeweza kuzungumza nao lakini hakuweza kufanya hivyo na mwishowe kujiona mjinga.
“Wakati wote nilikuwa nikijifikiria na kujiona mjinga, ni vipi nimepoteza muda wangu, unapokuwa mdogo huoni hilo leo ndicho kitu ninachowaambia watoto wangu, umuhimu wa elimu bora, kusoma na kujiandaa kwa lolote,” alisema Messi.
Messi alijiunga na klabu ya Barcelona akitokea kwao Argentina akiwa na miaka 13 na anakiri kwamba mwaka wake wa mwisho shuleni wakati akiwa Argentina ulikuwa wa hovyo kwani baada tu ya kumaliza shule alijiunga na akademi ya Barcelona maarufu La Masia.
Baada ya kuichezea kwa mafanikio Barcelona, Messi alijiunga na klabu ya PSG ya Ufaransa msimu wa 2020-21 na mwaka 2023 alijiunga na timu yake ya sasa ya Inter Miami inayoshiriki Ligi Kuu Marekani maarufu MLS.
