Cairo, Misri
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limelaani matukio yasiyokubalika yaliyojitokeza katika mechi kati ya Al Ahly ya Misti na AS FAR Rabat ya Morocco, mechi iliyochezwa Jumapili, Februari 15, 2026 na suala hilo limefikishwa kamati ya nidhamu.
Taarifa ya CAF iliyopatikana leo Jumatatu Februari 16, 2026 imeitaja mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiihusisha na vitendo hivyo ingawa haikufafanua ni vitendo gani visivyokubalika vilivyojitokeza katika mechi hiyo.
Katika mechi hiyo ya Kundi B, Al Ahly wakiwa nyumbani walitoka sare ya bila kufungana na AS Rabat, mechi ambayo ilichezwa wakati Ahly wakiwa na pointi tisa na tayari walikuwa wamefuzu kucheza robo fainali.
Kwa upande wa AS Rabat ili kufuzu hatua hiyo walihitaji sare ambayo waliipata na hatimaye kufikisha pointi tisa ambazo mpinzani wao mkuu Yanga hakuweza kuzipata licha ya kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 mbele ya JS Kablylie.
Kabla ya mechi hizo za mwisho za kundi hilo, Yanga walikuwa na pointi tano na AS Rabat pointi nane, matarajio ya Yanga yalikuwa ni Ahly ambao ni vinara wa kundi hilo wangepata ushindi na Yanga kumshinda Kabylie.
Matarajio hayo hata hivyo yalikwamishwa na matokeo ya sare ya Al Ahly na AS Rabat na kuufanya ushindi wa Yanga wa mabao 3-0 mbele ya JS Kabylie usiwe na maana yoyote kwa kuwa AS Rabat amefikisha pointi tisa.
Baadhi ya mashabiki hasa wanaoaminika kuwa wa Yanga walianza kutilia shaka mwenendo wa mechi ya AS Rabat na Ahly wengi wao wakiamini kuwa haikuwa na ushindani uliotarajiwa.
CAF katika taarifa yake ilieleza kuwa suala hilo limepelekwa kwenye kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo kwa ajili ya uchunguzi na hatua zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika katika vitendo hivyo.
Kimataifa Mechi ya Ahly, FAR Rabat yachunguzwa
Mechi ya Ahly, FAR Rabat yachunguzwa
Read also
