Na mwandishi wetu
Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Miguel Gamondi, hatimaye amesaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu hiyo baada ya kuwa kocha wa muda kwa takriban miezi mitatu sasa.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo kati ya Gamondi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilifanyika leo Jumatatu Februari 16, 2026 jijini Dar es Salaam kati ya Gamondi na Rais wa TFF, Walace Karia.
Miongoni mwa wageni waalikwa katika hafla hiyo ni Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda ambaye alithibitisha kuwa mshahara wa kocha huyo utalipwa na serikali akifafanua kuwa huo ni mojawapo ya uwekezaji wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye michezo.
Mara baada ya kusaini mkataba huo, Gamondi akionekana mwingi wa furaha alisema kwamba mkataba huo ni heshima kwake lakini pia ni changamoto ambayo ameahidi kukabiliana nayo.
Gamondi ambaye ana uzoefu wa soka la Afrika kwa zaidi ya miaka 20 pia ahidi kutumia nguvu zake kuijenga Taifa Stars isiyoogopa na yenye uwezo wa kupambana na timu bora za Afrika.
“Hili ni jukumu kubwa lakini niko tayari kulikabili, tukiwa wamoja na tukifata ushirikiano kutoka kwa wadau wote naamini tunaweza kupata matokeo yatakayowafanya Watanzania wawe na cha kujivunia,” alisema Gamondi.
Gamondi ambaye kwa hapa Tanzania amewahi kuzinoa timu za Yanga na Singida BS pia alitumia fursa hiyo kuipongeza serikali kwa uwekezaji katika soka pamoja na TFF kwa namna inavyowajibika kusukuma mbele maendeleo ya soka.
