London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema kitendo cha timu yake kuongoza Ligi Kuu England (EPL) kwa tofauti ya pointi tisa hakina maana yoyote licha ya timu hiyo kuzidi kuwapa presha mabingwa watetezi, Man City.
Jana Jumamosi Februari 7, 2026, Arsenal ilichapa Sunderland mabao 3-0 wafungaji wakiwa ni Martin Zubimenda na Viktor Gyokores aliyetupia kambani mara mbili na hivyo kujiimarisha kileleni kwa tofauti ya pointi tisa.
Man City ambao hawaonekani kulikatia tamaa taji hilo Jumapili hii watakuwa na kazi ya kujibu mapigo katika kuifukuzia Arsenal wakisaka ushindi wa ugenini katika mechi ngumu dhidi ya Liverpool.
Kwa mashabiki na baadhi ya wachambuzi wa soka tofauti ya pointi tisa inaonekana kuwa kubwa na yenye maana lakini alipoulizwa kuhusu tofauti hiyo, Arteta alisema kwamba haina maana yoyote.
“Bado tuna kazi ya kushinda mechi nyingi zaidi ili kufanikisha tunachokitaka , kwa hiyo tuache kuweka fikra zetu katika jambo hilo, tumefanya kazi nzuri leo (Jumamosi) tunayo ya kutuwezesha kufanya hivyo, kujitahidi kuwa bora zaidi na kuwa tayari kwa mechi ijayo dhidi ya Brentford,” alisema Arteta.
Badala yake, Arteta alitumia nafasi hiyo kumpongeza mchezaji wake Gyokores kwa namna ambavyo amekuwa bora baada ya kupitia wakati mgumu mwanzoni alipotua Arsenal majira ya kiangazi kwa ada ya Pauni 73.4 milioni akitokea Sporting Lisbon.
Arteta alisema anavutiwa na tabia za Gyokores na namna anavyouchukulia mchezo mmoja baada ya mwingine na utayari wake wa kutekeleza majukumu anayopewa uwanjani kwa ubora.
Alifafanua kuwa kinachomvutia zaidi kwa Gyokores ni namna ambavyo ameendelea kuwa katika ubora siku hadi siku jambo ambalo analionesha mazoezini, kuwaelewa vizuri wachezaji wenzake na kwenda vizuri na mchezo awapo uwanjani.
