Riyadh, Saudi Arabia
Sasa ni wazi kuwa siku za Cristiano Rinaldo katika klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia zinahesabika na zipo habari kwamba klabu hiyo imetangaza kuwa tayari kumuuza winga huyo kwa ada ya Pauni 42.9 milioni.
Ronaldo, 41, hatma yake katika klabu hiyo kwa siku za karibuni imekuwa katika sintofahamu hali ambayo imeonesha kuwa hana muda mrefu ataachana na klabu hiyo tajiri barani Asia.
Katika hali ambayo haikutarajiwa, Ronaldo kwa mara ya pili mfululizo aliachwa kwenye kikosi cha timu hiyo, kwanza aliikosa mechi ya Jumatatu iliyopita dhidi ya Al Riyadh na jana Ijumaa akaikosa mechi nyingine dhidi ya Al Ittihad.
Kukosekana kwa Ronaldo katika mechi hizo mbili kunatosha kuibua hisia kwamba kuna kitu kibaya kinaendelea kati ya Ronaldo na klabu hiyo na kilicho wazi ni kwamba wakati wowote atapewa mkono wa kwaheri.
Habari za ndani zinadai kwamba Ronaldo ameanza mgomo baridi akidaiwa kutoridhishwa na mfumo wa uendeshaji wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia maarufu Saudi Pro League.
Katika madai yake, Ronaldo ametaka ahakikishiwe kufanyika mabadiliko ya mfumo wa ligi hiyo jambo ambalo hajahakikishiwa na mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Real Madrid na Man United anaona kama amepuuzwa.
Al Nassr pamoja na kucheza bila Ronaldo, ilipata ushindi wa mabao 2-0 katika mechi dhidi ya Al Ittihad ingawa mashabiki walionekana kumuunga mkono Ronaldo kwa kuinua jezi na alama za rangi ya njano zenye picha ya mchezaji huyo.
Baada ya ushindi huo Al Nassr imepanda hadi nafasi ya pili katika ligi hiyo ikiwa nyuma ya vinara Al Hilal kwa tofauti ya pointi moja.
Wasimamizi wa Ligi Kuu Saudi Arabia, juzi Alhamisi walitoa taarifa wakimuonya Ronaldo kuwa hakuna mchezaji mwenye uwezo wa kushawishi maamuzi zaidi ya timu yake.
Kimataifa Siku za Ronaldo zahesabika Al Nassr
Siku za Ronaldo zahesabika Al Nassr
Read also
