London, England
Mshambuliaji wa zamani wa Man United, Wayne Rooney amesema anaamini kocha wa Arsenal, Mikel Arteta ali-paniki katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Man United, mechi ambayo Arsenal ililala kwa mabao 3-2.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili Januari 25, 2026 kwenye dimba la Emirates, Arsenal walikuwa wa kwanza kupata bao ambalo Lisandro Martinez alijifunga lakini mabao ya Bryan Mbeumo and Patrick Dorgu yaliifanya Man United kuwa mbele kwa mabao 2-1.
Rooney alisema kuwa katika mkakati wa kubadili mchezo, Arteta akaamua kufanya mabadiliko ya wachezaji lakini haikusaidia kitu ingawa walipata bao la kusawazisha kupitia kwa Mikel Merino mwisho wa siku bao la Matheus Cunha lilitosha kuipa Man United ushindi wa mabao 3-2.
Mpango wa Arteta katika mechi hiyo ni jambo ambalo Rooney amelitafsiri kuwa ni kupaniki hasa kwa namna alivyofanya mabadiliko ya wachezaji katika kipindi cha pili.
“Nafikiri Arteta yupo makini na nimekuwa nikimpongeza mara kadhaa lakini pia nafikiri alipaniki baada ya Man United kuwa mbele kwa mabao 2-1 na kufanya mabadiliko ya wachezaji wanne kwa mara moja,” alisema Rooney.
Rooney alisema kwamba anadhani alichopaswa kufanya Arteta kabla ya mabadiliko hayo ni kuiacha Arsenal ijaribu kurudi kwenye mchezo wake na wachezaji waliokuwa uwanjani badala ya kufanya kitu ambacho hakikumsaidia.
Mshambuiaji huyo wa zamani wa England hata hivyo alisema Arsenal bado ni timu yenya nafasi kubwa ya kubeba taji la ligi kuu lakini hadhani kama inaweza kubeba taji hilo kiurahisi.
