Na mwandishi wetu
Mambo si mazuri kwa Simba baada ya kuchapwa bao 1-0 na Esperance ya Tunisia katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa Jumamosi Januari 24, 2026 kwenye Uwanja wa Hammadi Agrebi mjini Rades.
Kwa matokeo hayo, Esperance wanashikilia usukani wa Kundi D wakiwa na pointi tano baada ya kucheza mechi tatu wakati Simba ikiendelea kuburuza mkia katika kundi hilo ambalo pia lina timu za Stade Malien ya Mali na Petro De Luanda ya Angola.
Bao pekee lililowapa ushindi wenyeji Esperance lilipatikana katika dakika ya 21 mfungaji akiwa ni Jacques Diarra baada ya kuiwahi pasi ndefu na kumzidi kasi beki wa Simba, Shomari Kapombe kabla ya kuujaza mpira wavuni.
Matokeo hayo pia yanazidi kufikisha matumaini ya Simba kucheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya klabu Afrika kwani hadi sasa timu hiyo imepoteza mechi zake zote tatu kati ya sita inazopaswa kucheza.
Kabla ya mechi ya Simba, mahasimu wao Yanga nao walikuwa ugenini Misri wakiumana na Al Ahly na Yanga kupoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 2-0.
Wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye michuano ya klabu Afrika, Jumapili hii Januari 25, 2026 wataingia katika viwanja tofauti kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam wakiwa wageni wa Nairobi United na Singida Black Stars watakuwa wenyeji wa AS Otoho ya Congo Brazzaville.
Kimataifa Esperance yailaza Simba 1-0
Esperance yailaza Simba 1-0
Read also
