Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amewajia juu waamuzi baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wolves na kudai kuwa alihitaji wachezaji wake wote bora wawepo ili kukabiliana na maamuzi hayo mabovu.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu England iliyopigwa Jumamosi Januari 24, 2026, Pep alichukizwa na kitendo cha mwamuzi Farai Hallam aliyekuwa akichezesha mechi yake ya kwanza ya ligi hiyo kuinyima Man City penalti.
Mwamuzi huyo alikataa ushauri uliotokana na mapitio ya VAR badala yake akashikilia msimamo wake wa uwanjani na kuinyima Man City penalti kwa madai kwamba mpira uligonga kwenye mkono wa mchezaji wa Wolves.
“Nilihitaji wachezaji wa kupambana dhidi ya uamuzi ule, tulishinda licha ya hilo, mechi ya mwanzo ya mwamuzi ilikuwa kubwa na sasa kila mmoja atamjua, nafikiri ni kwa mara ya kwanza wanakwenda kwenye VAR na kukataa kitu ambacho kilionekana wazi yaani kwenye mikono,” alisema Pep.
Pep alisema kwamba ana uhakika bosi wa waamuzi Howard Webb Jumapili atalazimika kuzungumza na waandishi wa habari ili kuelezea ni kwa nini ile haikuwa penalti.
“Nasubiri kesho (Jumapili) tusisubiri hadi Jumatano kwa sababu tuna mechi ya ligi ya mabingwa, tuna mambo mengi, Howard Webb njoo kesho (Jumapili) na ueleze ni kwa nini ile si penalti na ndio maana nikawataka wachezaji wapiganie kile ambacho tumekuwa tukikipigania tangu siku ya kwanza,” alisema Pep.
