London, England
Mshambuliaji wa Arsenal, Bukayo Saka amekubali kuongeza mkataba na klabu hiyo huku ikidaiwa kwamba mkataba huo mrefu utamfanya awe mmoja wa wachezaji wenye mshahara mkubwa.
Saka, 24, anakuwa sehemu ya mpango maalum wa Arsenal kuhakikisha wanaendelea kubaki na wachezaji wao mahiri wa kuisaidia timu hiyo katika mbio za kulisaka taji la Ligi Kuu England na mataji mengine wanayoyawania.
Wachezaji wengine ambao tayari walishaongeza mikataba yao katika kipindi cha majira ya kiangazi ni Myles Lewis-Skelly, Gabriel Magalhaes, Ethan Nwaneri pamoja na William Saliba.
Saka ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya England, amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kwanza cha Arsenal tangu ajiunge na timu hiyo mwaka 2018 akiwa amepitia katika akademi ya timu hiyo hiyo.
Msimu uliopita, Saka aliifungia Arsenal mabao 12 na kutoa asisti 13 katika mechi 36 alizochezea timu hiyo ingawa alipitia wakati mgumu na kujikuta akisugua benchi kwa takriban miezi mitatu kutokana na tatizo la misuli.
Habarai za mkataba mpya hata hivyo hazikuweka wazi kuhusu miaka ambayo Saka ataongeza katika mkataba wake wa sasa badala yake ilielezwa tu kuwa amekubali kuongeza mkataba ambao utamfanya aendelee kuwa na klabu hiyo kwa muda mrefu zaidi.
Arsenal imepania kulibeba taji la ligi kuu msimu huu baada ya kulipigania kwa muda mrefu na kwa sasa timu hiyo inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi sita huku ikiwa na rekodi nzuri za ushindi kwa mechi za hivi karibuni.
Kimataifa Saka kuongeza mkataba Arsenal
Saka kuongeza mkataba Arsenal
Read also
