Na Hassan Kingu
Timu ya taifa ya Morocco imekamilika kila idara, historia yake inatisha, si Afrika tu bali duniani kote, tayari imeonesha ubora wake kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 kwa kufika hatua ya nusu fainali.
Unapozungumzia Kombe la Dunia maana yake ni kwamba unazungumzia mashindano makubwa ya soka duniani, Morocco wameonesha ubora wao katika michuano hiyo na kuingia katika orodha ya timu tishio.
Morocco ni timu ya kwanza barani Afrika kufikia nusu fainali ya Kombe la Dunia, hii ni rekodi ya kipekee na ya kujivunia si kwa Morocco tu bali hata Shirikisho la Soka Afrika (CAF) linajivunia rekodi hiyo.
Katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazoendelea nchini Morocco, wenyeji hao Morocco ni timu inayopewa nafasi kubwa kama si nafasi ya kwanza kubeba taji hilo au kulibakisha nyumbani.
Morocco hiyo ambayo inatisha Afrika yenye rekodi za kutisha kuanzia kwenye Afcon yenyewe, Jumapili hii ya Januari 4, 2026 itacheza na timu ya taifa ya Tanzania au Taifa Stars, timu ambayo haikuwamo katika timu zinazopewa nafasi ya japo kufikia hatua ya robo fainali.
Si robo fainali tu, Taifa Stars haikuwamo hata katika timu ambazo ungeweza kuzitaja kuwa zitavuka hatua ya makundi, ni timu ambayo ilihusishwa na mechi tatu za makundi na baada ya hapo kurudi nyumbani.
Kilichotokea ni tofauti na matarajio ya wengi, hata baadhi ya mashabiki wachache wa Tanzania ambao pengine hawakupenda kuona timu hiyo inafanikiwa wameshangazwa na hatua ambayo timu imefikia.
Huenda hata wachezaji wenyewe hawakutarajia kama wangefanya vizuri kiasi cha kufuzu kucheza hatua ya mtoano (16 bora) na hilo linathibitishwa na hali ya furaha waliyokuwa nayo baada ya kufuzu kiasi cha kuimba kibao cha ‘Sisi ndio wale wale mliotukataa mkasema hatufiki mbali…’
Kimsingi Taifa Stars iliingia katika Afcon ikiwa kile kinachoitwa ‘underdogs’ unaweza kusema ni timu dhaifu lakini leo imepiga hatua na sasa inasubiri kukabiliana na Morocco au miamba ya soka barani Afrika.

Wanachokutana nacho Stars leo kinanikumbusha tukio la mwaka 2012, timu ya taifa ya Zambia ikiwa chini ya kocha Mfaransa, Renard Herve ililishangaza bara la Afrika, haikuwa timu iliyotajwa au kupewa nafasi ya kufika mbali, mafanikio pekee ambayo ilihusishwa nayo ni kupambana hadi kufika hatua ya robo fainali.
Hali ikawa tofauti, Zambia au Chipolopolo (pichani) ilipiga hatua moja baada ya nyingine ikiwapangua vigogo na mwishowe ikafika fainali na kubeba taji hilo katika michuano iliyofanyika Guinea ya Ikweta na Gabon.
Katika fainali za 2012 kuna ukweli kwamba baadhi ya nchi mahiri katika soka Afrika zilikuwa na matatizo ya kisiasa kuanzia Misri, Libya na Algeria, hapo hapo timu za Nigeria, Afrika Kusini na Cameroon zilishindwa kufuzu.
Kwa baadhi ya wachambuzi hali hiyo ilijengewa hoja kwamba ndio sababu mojawapo ya Zambia kufanya vizuri hadi kubeba taji la michuano hiyo lakini kimsingi kilichowawezesha Zambia kubeba taji ni uwezo na kujiamini kwa wachezaji.
Kujiamini huko ndiko kulikoifanya timu hiyo ipenye hadi kubeba taji katika michuano ambayo pia ilishirikisha mataifa mengine mahiri katika soka la Afrika kuanzia Morocco, Senegal na wenyeji Guinea na Gabon.
Kubwa kuliko yote ni ushindi wao katika mechi ya fainali dhidi ya Ivory Coast, taifa ambalo lina heshima yake katika soka la Afrika na kabla ya mechi ndiyo timu iliyotajwa na wachambuzi na hata wacheza kama kuwa ndiyo ambayo ingebeba taji hilo na kuwa taji lao la nne kwa wakati huo.
Hali hata hivyo ikawa kinyume, Zambia wakaishangaza Afrika, wakawashangaza wachambuzi na wacheza kamari, wakaushangaza ulimwengu kwa kutoka sare na Ivory Coast kabla ya kuwatoa kwenye penalti na kubeba taji.
Sijui ni kwa nini na huenda si mimi peke yangu, historia ya Chipolopolo hadi kuibwaga Ivory Coast na kubeba taji la Afcon 2012 inanifikirisha wakati huu Taifa Stars ikijiandaa kuikabili Morocco.
