Rabat, Morocco
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa mara ya kwanza imeingia hatua ya mtoano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Tunisia, mechi iliyochezwa leo Jumanne, Desemba 30, 2025.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kufikia hatua hiyo baada ya kuishia hatua ya makundi katika fainali zote ilizofuzu kuanzia mwaka 1980 ilipofuzu kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Mechi dhidi ya Tunisia ndiyo ya mwisho kwa Stars katika mechi zake za Kundi C na imemaliza ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Nigeria iliyoshika usukani, Tunisia ya pili na Uganda ikiburuza mkia katika kundi hilo.
Stars imemaliza na pointi mbili, Nigeria tisa na Tunisia nne wakati Uganda haina pointi hata moja na kuiacha Stars ikifuzu kupitia kundi la best loosers na sasa inasubiri kuumana na wenyeji Morocco.
Tunisia ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 42 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Ismail Gharbi baada ya Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ kumkaba shingoni Hazem Mastouri wa Tunisia aliyekuwa akiuwahi mpira wa juu uliopigwa na Hannibal Mejbri kuelekea kwenye lango la Stars.
Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi Jacques Ndala Ngambo baada ya kujiridhisha kupitia VAR na picha kurudiwa zikimuonesha Bacca alivyomzuia Mastouri kwa kumkaba shingoni ndani ya eneo la penalti na mwamuzi kumpa kadi ya njano beki huyo wa Yanga.
Stars walisawazisha bao hilo dakika ya 54 mfungaji akiwa Feisal Salum au Fei Toto ambaye alifumua shuti la chinichini akiwa nje ya eneo la 18 na kumuacha kipa wa Tunisia, Aymen Dahmen akiruka bila mafanikio.
Tunisia waliuanza mchezo vizuri wakitawala kila eneo na Stars kujikuta wakifanya kazi ya kuzuia mashambulizi na katika dakika ya 11, Gharbi alifumua shuti lililogonga mwamba wa juu kwenye kona na kurudi uwanjani na kuwaacha mashabiki wa Stars wakiwa hawaamini kilichotokea.
Kipa wa Stars, Hussein Masalanga aliruka akijaribu kuufuata mpira huo lakini aliishia kuuangalia kwa macho ukigonga mwamba kabla ya kurudi uwanjani.

Stars nao walianza kujiamini huku Mbwana Samatta na Simon Msuva wakionekana kuwa tishio kwenye lango la Tunisia ambao hatimaye walianza kucheza kwa tahadhari zaidi.
Kocha wa Stars, Miguel Gamondi ambaye timu yake ilianza mchezo kwa kujihami, kipindi cha pili alionekana kubadili mbinu ambazo zilisaidia kuifanya Stars icheze pasi na kulisogelea lango la Tunisia mara kadhaa na haikushangaza kwa timu hiyo kupata bao.
Katika kipindi hicho, Gamondi alianza kwa kumtoa Samatta na nafasi yake kuingia Seleman Mwalimu, baadaye akamtoa Mohamed Hussein Zimbwe na kuingia Paschal Msindo.
Mabadiliko hayo yaliendelea kwa kuwatoa, Fei Toto, Msuva na Haji Mnoga na nafasi zao kuingia Charles M’mombwa, Tarryn Allarakhia na Shomari Kapombe.
Stars sasa ina kazi ngumu ya kuwakabili wenyeji Morocco, mechi ambayo itachezwa Jumapili ijayo ya Januari 4, 2026 wakati siku moja kabla Tunisia wao wataumana na Mali.
