Manchester, England
Kiungo wa Man United, Bruno Fernandes amesema Cristiano Ronaldo bado ana mchango mkubwa kwa timu ya taifa ya Ureno na hakubaliani na wanaodai kuwa timu hiyo inacheza vizuri ikimkosa mchezaji huyo.
Katika mechi ya hivi karibuni, Ureno ikiwa bila ya Ronaldo aliyekuwa akitumikia adhabu ilipata ushindi wa mabao 9-1 dhidi ya Armenia na hatimaye kufuzu moja kwa moja kucheza fainali za Kombe la Dunia 2026.
Fernandes ambaye pia ni nahodha wa Man United, pamoja na matokeo ya mechi dhidi ya Armenia hata hivyo bado anaamini Ronaldo akiwa ndani ya eneo la boksi anabaki kuwa mchezaji wa kiwango cha juu.
“Ronaldo anawachanganya mabeki na kutengeneza nafasi kwa wachezaji wengine,” alisema Fernandes akimpamba mchezaji huyo mkongwe aliyewahi kuzichezea Man United na Real Madrid.
Akifafanua zaidi Fernandes alisema anatambua kile watu wanachofikiria kwamba huwa wanacheza vizuri na kuwa huru bila ya Ronaldo lakini kama hilo linatokea tatizo ni wao wenyewe kwani hawatakiwi kuwa na hofu Ronaldo anapokuwa uwanjani kwa sababu mchezaji huyo anaweza kuwapa vitu zaidi.
Nafasi ya Ronaldo kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Ureno ilianza kuwa mashakani baada ya kuwekwa benchi na kocha Fernando Santos kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022.
Mambo hata hivyo yalibadilika kwa mchezaji huyo wa Al Nassr ya Saudi Arabia baada ya kuanza tena kuonesha makali yake kwa mara nyingine timu ikiwa chini ya kocha Roberto Martinez.
Ronaldo, 40, ambaye alianza kuichezea timu ya taifa ya Ureno kwa mara ya kwanza mwaka 2003, kwa sasa ndiye mchezaji anayeongoza kwa kuifungia mabao mengi timu hiyo, mabao 143 katika mechi 226.
