Paris, Ufaransa
Mahakama ya Kazi nchini Ufaransa imeitaka klabu ya PSG kumlipa mshambuliaji wake wa zamani, Kylian Mbappe fidia ya Pauni 52 milioni ikiwa ni malimbikizo ya mishahara na marupurupu.
Mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa anaichezea Real Madrid katika madai yake ya awali aliyoyafikisha katika mahakama hiyo ya mjini Paris alitaka alipwe Pauni 231 milioni huku PSG nao wakifungua kesi kudai fidia ya Pauni 211 milioni.
Katika madai ya awali Mbappe alikuwa akiidai PSG fidia kwa kuchafuliwa jina katika mgogoro wa mkataba wake na klabu hiyo na namna ambavyo klabu haikumpa heshima lakini mahakama iliamua alipwe sehemu ya alichodai.
Inaaminika kuwa sehemu kubwa ya fedha ambazo mahakama imetaka mshambuliaji huyo alipwe ni za marupurupu na si mshahara ambapo awali mahakama ilizuia akaunti za PSG baada ya maombi ya mawakili wa Mbappe.
“Tumeridhishwa na uamuzi huu, hiki ndicho unachokitarajia pale ambapo mishahara hailipwi, uamuzi wa aina hii unaonesha ni kwa kiasi gani makubaliano yanapofikiwa ni lazima yatekelezwe,”ilieleza taarifa ya mawakili wa Mbappe.
Wakati timu ya mawakili wa Mbappe ikionekana kuridhishwa na uamuzi wa mahakama, upande wa PSG hakufuta uwezekano wa kuukatia rufaa uamuzi huo.
PSG imekuwa ikidai kulipwa Pauni zaidi ya 290 milioni ikiwa ni fidia katika mpango wa mwaka 2023 wa uhamisho wa Mbappe kwenda Saudi Arabia kujiunga na klabu ya Al Hilal, uhamisho ambao ulikwama.
Badala yake Mbappe alihamia Real Madrid akiwa mchezaji huru na sasa PSG wamepokea uamuzi wa Mahakama ya Kazi ya Paris na wanajipanga kufanyia kazi uamuzi huo wakitambua kwamba wana haki ya kukata rufaa.
