Riyadh, Saudi Arabia
Mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Karim Benzema amesema kocha wa timu hiyo Xabi Alonso hapaswi kulaumiwa kwa matokeo yasiyoridhisha badala yake amewanyooshea kidole wachezaji.
Alonso Jumapili hii Desemba 14, 2025, timu yake itaingia uwanjani kuumana na Alaves wakati ambao kuna presha kubwa ya kutaka kutimuliwa kwa kocha huyo kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya mechi za karibuni.
Real Madrid ikiwa nyumbani wiki iliyopita ililala kwa mabao 2-0 mbele ya Celta Vigo katika mechi ya La Liga na Jumatano iliyopita ilichapwa mabao 2-1 na Man City katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Benzema ambaye amefanikiwa kubeba mataji kadhaa katika miaka 14 aliyoichezea Real Madrid kabla ya kuhamia Al Ittihad ya Saudi Arabia Julai mwaka juzi amesema kocha hawezi kufanya lolote kwani ana wachezaji wenye majina makubwa.
“Wanachokosa ni muunganiko kati ya Mbappe (Kylian), Vinicius, Bellingham na Rodrygo, kila mmoja anatakiwa ajue nini anafanya uwanjani, Bellingham anatakiwa kuelewa kwamba yeye ni kiungo mshambuliaji si mfungaji mabao, Mbappe ni mfungaji mabao si kiungo mshambuliaji, Vinicius si kiungo mkabaji ni winga wa kushoto” alisema Benzema.
Benzema ambaye pia ameichezea timu ya taifa ya Ufaransa aliongeza kwa kusema kuwa iwapo wachezaji hao watajua wanachotakiwa kufanya uwanjani kila kitu kitakuwa sawa.
“Hiyo ni kwa sababu tunawazungumzia wachezaji ambao ni kati ya wachezaji 10 bora duniani na wote wapo kwenye timu moja,” alisema Benzema.
Benzema, 37, ambaye alicheza Real Madid iliyokuwa na kina Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na mastaa wengineo alisema Mbappe ambaye ana mabao 25 katika mechi 21 anahitaji kubeba jukumu la kiuongozi kwenye kikosi hicho
Kwa mujibu wa Benzema hakuna mchezaji mwingine mzoefu anayeweza kumwambia Bellingham, Mbappe au Vinicius kwamba anafanya kitu ambacho si sahihi na hapo ndipo anapoamini kuna utata kwani na kocha kalisema hilo kwa namna tofauti.
“Wachezaji hawa hawazungumzi, inaonesha hivyo, ni kama vile nimefanya kazi yangu, nafunga mabao, hilo ndilo soka la zama hizi lakini kama mchezaji mwenzako ni bora kukuzidi unatakiwa kukubali hilo,” alisema Benzema.
