Washington, Marekani
Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), imetakiwa kumchunguza rais wa shirikisho hilo, Gianni Infantino akituhumiwa kuvunja kanuni ya kutojihusisha na siasa kutokana na uhusiano wake na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Wiki iliyopita, Infantino alimpa Trump, 79, tuzo ya Fifa ya amani wakati wa hafla ya droo ya fainali za Kombe la Dunia 2026 na hapo hapo ameonesha kumuunga mkono kiongozi huyo wa Marekani katika mahojiano aliyofanya kwenye mitandao ya kijamii.
Taasisi inayojihusisha na utetezi wa haki za binadamu ya FairSquare imeandika barua ya malalamiko ikidai kuwa Infantino amevunja kanuni nne za Fifa kuhusu kutojihusisha na upande wowote katika siasa.
Infantino alikuwa sambamba na Trump kwenye ukumbi wa Kennedy katika hafla ya droo hiyo kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia 2026 ambazo zitafayika Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 mwakani.
“Tuzo ya aina ile kwa kiongozi wa kisiasa aliye madarakani yenyewe tu ni uvunjaji wa wazi wa kanuni za Fifa kuhusu kutojihusisha na upande wowote,” ilieleza sehemu ya barua ya FairSquare.
Kwa mujibu wa FairSquare, rais wa Fifa hana mamlaka ya kuamua yeye mwenyewe kuhusu dira, muelekeo, sera na taratibu za Fifa.
Sambamba na tuzo hiyo ya dhahabu, Infantino pia alimzawadia Trump medali na cheti na katika hotuba yake bosi huyo wa Fifa akasema hicho ndicho wanachokitaka kwa kiongozi na kumuhakikishia Trump kwamba atamuunga mkono.
Oktoba mwaka jana Infantino, 55, alinukuliwa akisema kwamba Trump anahaki ya kupewa tuzo ya nobeli jambo ambalo liliibua mjadala na kuongeza kuwa Trump anatakiwa kuungwa mkono na wote.
“Wote tunatakiwa kuunga mkono anachofanya Trump, ni kwa sababu nadhani ni jambo linaloonekana kuwa zuri,” alisema Infantino.
