Manchester, England
Mshambuliaji wa Manchester United, Benjamin Sesko (pichani) anatarajia kurudi uwanjani hivi karibuni baada ya kuwa majeruhi wa goti.
Sesko, 22, amekuwa nje ya uwanja akisumbuliwa na maumivu ya goti aliyoyapata Novemba 8 mwaka huu katika mechi dhidi ya Tottenham Hotspur iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
Kwa kipindi chote hicho, Sesko ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Slovenia aliyejiunga na Man United majira ya kiangazi msimu huu akitokea RB Leipzig ya Ujerumani, amekosa mechi nne za Ligi Kuu England.
Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa kwa ada ya Dola 98 milioni, Man United wanamhitaji zaidi wakati huu ambao mastaa wake Bryan Mbeumo na Amad Diallo watajiunga na timu zao za taifa kwa ajili ya fainali za Afcon.
Hadi sasa kocha wa Man United, Ruben Amorim hajaweka wazi ni siku gani hasa ambayo Sesko atarejea dimbani lakini kwa mujibu wa wakala wake, mchezaji huyo atakuwa fiti wakati wowote katika siku za karibuni.
“Benjamin (Sesko) anajiona katika hali nzuri, matibabu yake yanakwenda kama yalivyopangwa, ana shauku kubwa ya kurejea uwanjani, anajiona ame-miss kucheza soka na katika hilo kidogo ni kama anachoka kusubiri, kwa hiyo ni matumaini atakuwa vizuri hivi karibuni,” alisema wakala wa mchezaji huyo.
Sesko ambaye hadi sasa amefunga mabao mawili kwenye Ligi Kuu England katika mechi 11, alisajiliwa Man United pamoja na Mbeumo na Matheus Cunha hatua ambayo ilikuwa ya kuijenga upya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
