Liverpool, England
Mshambuliaji wa zamani wa Man United na timu ya taifa ya England, Wayne Rooney amemtaka kocha wa Liverpool, Arne Slot kumtupa benchi mshambuliaji wake Mohamed Salah kama njia ya kusaka ubora katika timu.
Rooney ametoa kauli hiyo baada ya matokeo ya Jumamosi ambapo Liverpool ilichapwa mabao 3-0 na Nottingham Forest na hivyo kuishusha timu hiyo hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Katika mechi hiyo, Salah alishindwa kutoa asisti au kufunga bao katika kipigo hicho ambacho ni cha sita katika mechi saba za ligi hiyo zilizopita.
Rooney ambaye pia amewahi kuwa kocha lakini hakupata mafanikio, katika hoja yake dhidi ya Salah alisema kwamba mchezaji huyo hana msaada kwa timu hata kwenye ulinzi.
Rooney alisema suala hilo linaweza kuwa linawagusa hata wachezaji wengine waliosajiliwa ambao wapo kwenye benchi na wanamuona si mwenye kukimbia kama inavyotakiwa.
“Kama mimi ningekuwa Arne Slot ningejaribu kufanya maamuzi makubwa ili yawe na matokeo chanya kwa timu yote, unapokuwa hushindi mechi unatakiwa kuwa mpambanaji na mgumu kushindwa,” alisema Rooney.
Rooney alisema Slot anatakiwa kufanya maamuzi ya kuwafanya wachezaji wawe wapambanaji na wasioshindwa na kila mchezaji awe anakimbia na watakapoanza kushinda mechi anaweza kumrudisha kwenye timu na kuwa mwenye bidii zaidi.
Sambamba na Salah ambaye amewahi kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo, Rooney pia aliwagusia wachezaji wengine wakongwe kwenye timu akiwamo nahodha Van Dijk akisema kuwa hawapo katika ubora kama ilivyokuwa msimu uliopita na hawaisaidii timu.
Rooney pia alisema kwamba huenda kifo cha mchezaji mwenzao Diogo Jota kilichotokana na ajali ya gari kimechangia kuharibu mambo katika timu hiyo ambayo alisema inapitia wakati mgumu.
