Na mwandishi wetu
Simba imeanza vibaya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuchapwa bao 1-0 na Atlético Petroleos de Luanda ya Angola katika mechi iliyopigwa Jumapili Novemba 23, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Bao pekee lililoizamisha Simba katika mechi hiyo lilifungwa na Bernado Dias baada ya kupiga shuti ambalo lilimbabatiza Rushine de Reuck na mpira kujaa wavuni.
Simba licha ya kutoka uwanjani vichwa chini lakini timu hiyo ilionesha uhai na kutengeneza nafasi kadhaa mfano ni dakika ya 52 Elly Mpanzu akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga alipiga shuti lisilo na macho.
Msimu uliopita Simba ilifikia hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho na msimu huu imekuwa ikipewa matumaini makubwa ya kufika mbali ingawa baada ya matokeo haya, timu hiyo sasa itakuwa na kazi ya kufanya katika mechi nyingine za Kundi D.
Kushindwa huko kwa Simba kunakuwa pigo la tatu kwa timu za Tanzania kwenye michuano ya klabu barani Afrika baada ya Azam FC na Singida Black Stars nao kupoteza mechi zao za makundi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Azam walishindwa kutamba mbele ya Maniema Union ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kuchapwa mabao 2-0 wakiwa ugenini wakati Singida pia wakiwa ugenini walifungwa mabao kama hayo na CR Belouizdad ya Algeria.
Timu pekee ya Tanzania iliyoanza na mguu mzuri mechi zake za makundi ni Yanga ambayo Jumamosi ya Novemba 22, 2025 ikiwa kwenye dimba la New Amaan, Zanzibar ilitoka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya FAR Rabat ya Morocco.
Kimataifa Simba yaanza vibaya makundi Afrika
Simba yaanza vibaya makundi Afrika
Read also
