Na mwandishi wetu
Prince Dube, mshambuliaji wa Yanga aliyekuwa akiandamwa na ukame wa mabao hatimaye amefuta ukame huo kwa kufunga bao pekee na la ushindi kwa timu yake iliyokuwa ikiumana na FAR Rabat ya Morocco.
Ushindi huo uliopatikana leo Jumamosi Novemba 22, 2025 kwenye dimba la New Amaan, Zanzibar inakuwa karata muhimu kwa Yanga katika mbio za kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Afrika.
Bao hilo pekee la Yanga lilipatikana dakika ya 59 baada ya Dube kuizidi ujanja safu ya ulinzi na kuutumia vyema mpira uliotoka kwa Mudathir Yahya kabla ya kufumua shuti lililojaa wavuni.
Hilo linakuwa bao la kwanza kwa Dube msimu huu baada ya kupitia wakati mgumu akiandamwa na ukame wa mabao hali iliyoibua uvumi kwamba huenda angeachana na Yanga.
Bao hilo lilipokelewa kwa shangwe na mashabiki wa Yanga kwa kuamini kuwa timu yao imeanza vyema hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati huo huo ikiwa kama mwanzo mpya wa kuzifumania nyavu kwa Dube.
Yanga iliendelea kuonesha juhudi za kusaka bao la pili na dakika tano baada ya bao la Dube, Maxi Nzengeli nusura aipatie Yanga bao la pili lakini mpira wa kichwa alioupiga uliokolewa na kipa wa FAR Rabat.
Wakati Yanga wakionekana kusaka bao la nyongeza, wapinzani wao ni kama walitumia muda mwingi kuwasoma, wakimiliki mpira na kujihami huku wakipeleka mashambulizi machache kwenye lango la Yanga lililolindwa na kipa Djigui Diara.
Ushindi wa leo pia ni mwanzo mzuri kwa kocha wa Yanga, Pedro Concalves kwenye michuano ya kimataifa tangu akabidhiwe nafasi hiyo hivi karibuni baada ya kutimuliwa kwa Romain Folz.
Kimataifa Dube awatungua FAR Rabat
Dube awatungua FAR Rabat
Read also
