Manchester, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim (pichani) ana matumaini ya kufikia makubaliano na mashirikisho ya soka ya Cameroon, Morocco na Ivory Coast ili wachezaji wao wachelewe kujiunga na timu za taifa kwa ajili ya Afcon 2025.
Wachezaji walengwa katika mpango huo wa Amorim ni Bryan Mbeumo wa Cameroon, Noussair Mazraoui wa Morocco na Amad Diallo wa Ivory Coast ambao timu hiyo itawakosa wakati wa michuano hiyo ya mataifa ya Afrika inayoanza Desemba 21 na kufikia tamati Januari 18.
Amorim anafahamu fika kwamba wachezaji hao watatu watatakiwa na timu zao za taifa wiki mbili kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ingawa anaamini makubaliano yanaweza kufikiwa ili wachelewe kidogo.
Man United inajipanga ili iwe na kikosi imara kadri iwezekanavyo katika mechi yake dhidi ya Wolves ambayo itachezwa Desemba 8 na baada ya hapo Desemba 15 itakuwa nyumbani Old Trafford dhidi ya Bournemouth.
“Tunajaribu kuangalia uwezekano wa kuwa na wachezaji kwa muda mrefu zaidi lakini tutaona itakavyokuwa nadhani ni wiki mbili kabla ya kuanza kwa mashindano, tutajaribu kuandaa kitu na mashirikisho, tunajua kuhusu Afcon, ni nafasi kwa wachezaji wengine lakini hao ni wachezaji wetu muhimu,” alisema Amorim.
Hali imekuwa mbaya zaidi kwa Man United hasa baada ya kuumia kwa mshambuliaji Benjamin Sesko ambaye naye ataikosa mechi ya ugenini Jumatatu ijayo dhidi ya Everton.
Kwa upande wake Amorim amesema tatizo la goti linalomsumbua Sesko ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Slovenia, si kubwa sana lakini atakosekana uwanjani kwa wiki kadhaa.
