Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars chini ya kocha wake mpya, Miguel Gamondi imelala kwa mabao 4-3 mbele ya Kuiwat ikiwa mechi ya kwanza kwa timu hiyo chini ya kocha huyo mpya.
Katika mechi hiyo ya kimataifa ya kirafiki iliyochezwa Jumamosi hii Novemba 15 mjini Cairo, Misri kwenye Uwanja wa Al Salam, Stars walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0.
Mabao ya Stars yalifungwa na Charles M’mombwa dakika ya sita wakati bao la pili lilifungwa na Tarryn Allarakhia katika dakika ya 34.
Mambo yalianza kuwaharibikia Stars kipindi cha pili baada ya Kuwait kufunga mabao mawili yaliyofungwa dakika za 46 na 53 mfungaji akiwa ni Mohammad Daham aliyefunga yote mawili.
Bao la tatu la Kuwait lilifungwa na Yousef Nasser dakika ya 64 na la nne lilifungwa na Hassan Hamdan dakika ya 69 wakati bao la tatu la Stars lilifungwa na M’mombwa ambaye alifunga mawili.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha wa Stars, Gamondi aliisifu timu yake kwa kucheza vizuri kipindi cha kwanza lakini akalalamikia hali ilivyokuwa kipindi cha pili hasa baada ya kuruhusu mabao matatu.
Gamondi pia alisema yake huenda iliathiriwa na kukosa umakini na uzoefu hapo hapo akasisitiza umuhimu wa kuyaangalia na mambo mazuri ambapo alisifia upambanaji wa wachezaji wake hadi hatua ya mwisho.
Naye beki na nahodha wa Stars, Shomari Kapombe alisifia uchezaji wao hasa kwa kipindi cha kwanza na kukiri kwamba kipindi cha pili walipoteana na kupoteza mawasiliano hadi kuruhusu mabao mawili ya haraka.
Kimataifa Kuwait yaipiga Taifa Stars 4-3
Kuwait yaipiga Taifa Stars 4-3
Read also
