Na mwandishi wetu
Utani wa klabu kongwe za soka nchini Simba na Yanga sasa umehamia kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mashabiki wa Simba kujinasibu kwa kumpata spika na Yanga wakijinasibu kwa kumpata waziri mkuu.
Katika Bunge jipya lililotokana na uchaguzi mkuu wa 2025, Mussa Azan Zungu anayefahamika kuwa shabiki wa Simba ameteuliwa kuwa Spika wa bunge hilo wakati shabiki wa Yanga, Mwigulu Nchemba amechaguliwa kuwa waziri mkuu.
Jina la Mwigulu aliyekuwa waziri wa fedha, kwa mashabiki wa Yanga linakuwa furaha kwao kwa kuwa waziri mkuu aliyepita Kassim Majaliwa alifahamika kuwa shabiki mkubwa wa mahasimu wao Simba.
Kwa upande wa Simba mashabiki wa timu hiyo ni kama vile wana zali na nafasi ya spika ambayo mashabiki na wapenzi wa timu hiyo wamekuwa wakiishika mara kwa mara.
Ukianzia kwa Samwel Sitta, huyu ungeweza kumwita kuwa shabiki kindakindaki wa timu hiyo na japo alikuwa havumi lakini wanaomjua wanakiri kwamba aliipenda Simba na kuhusishwa na mambo kadha wa kadha.
Sitta ambaye kwa sasa ni marehemu, inadaiwa ushabiki wake haukuishia katika kujinasibu tu bali hata misaada alikuwa akitoa pale Simba ilipokwama na inadaiwa miaka ya nyuma alichangia ujio wa makocha kutoka Brazil walioinoa timu hiyo.
Sitta pia inadaiwa akiwa mtumishi wa serikali, ni mmoja w watu waliotoa mchango mkubwa miaka ya nyuma kufanikisha safari ya timu hiyo kwenda Brazil, taifa linalosifika kwa kuwa na historya ya kipekee katika soka.
Baada ya Sitta, nafasi ya spika ilishikwa na Anna Makinda, huyu japo hakujulikana lakini wapo waliodai kwamba ana ushabiki wa Simba kama ilivyokuwa kwa Job Ndugai ambaye alikuwa spika baada ya Makinda.
Ndugai ambaye kwa sasa ni marehemu hakuwa mwenye kujizuia kutoa vijembe vya hapa na pale bungeni pale Simba ilipofanya vizuri lakini hata alipoachia kiti hicho, aliyemfuata Dk Tulia Ackson naye anafahamika kuwa na mapenzi na klabu ya Simba.
Baada ya Tulia ambaye amewahi kuonekana na jezi ya timu hiyo mara kadhaa, kiti hicho kimekabidhiwa kwa Zungu, mbunge wa Ilala ilipo klabu ya Simba na kwa muda mrefu amekuwa akidhihirisha mapenzi yake na klabu hiyo ya mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Soka Spika Simba, Waziri Mkuu Yanga
Spika Simba, Waziri Mkuu Yanga
Related posts
Read also
