Porto, Ureno
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, amethibitisha kuwa fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakuwa za mwisho kwake.
Ronaldo, nyota wa zamani wa timu za Sporting Lisbon, Man United, Real Madrid na Juventus kwa sasa ana miaka 40 akiwa na rekodi ya kufunga mabao 952 kwa klabu alizochezea na timu yake ya taifa, pia amesema atastaafu soka mwaka mmoja au miwili ijayo.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika katika nchi za Canada, Mexico na Marekani na kama Ronaldo atakuwamo kwenye fainali hizo basi atakuwa ameweka rekodi ya kushiriki fainali za michuano hiyo mikubwa ya soka duniani kwa mara sita.
Ronaldo ambaye kwa sasa anaichezea Al Nasr ya Saudi Arabia anashika nafasi ya kwanza kwa kuwa mchezaji mwenye rekodi ya kufunga mabao mengi katika mechi za kimataifa, mabao 143.
Akijibu swali aliloulizwa iwapo atastaafu baada ya Kombe la Dunia 2026, Ronaldo alijibu kwa kifupi akisema ndio huo utakuwa mwisho wake katika tukio hilo kubwa (Kombe la Dunia) na hapo hapo akazungumzia kustaafu soka moja kwa moja.
“Ndio, hilo ni wazi, wakati huo nitakuwa na miaka 41 na nafikiri huo utakuwa mwisho katika michuano mikubwa, na pia ngoja tu niwe wazi, nikisema hivi karibuni namaanisha mwaka mmoja au miwili bado nitakuwa kwenye mchezo huu (soka),” alisema Ronaldo.
Ronaldo pamoja na kuwa kwenye soka kwa kipindi kirefu na kubeba mataji na tuzo mbalimbali kubwa, hajaweza kubeba Kombe la Dunia, mafanikio pekee makubwa kwa timu yake ya taifa ni yale ya mwaka 2016 alipobeba taji la Euro na timu ya Ureno.
Ureno hata hivyo hadi sasa bado haijawa na uhakika wa kucheza fainali za Kombe la Dunia 2026 na ili kupata nafasi hiyo italazimika kupata ushindi katika mechi yao ya Alhamisi dhidi ya Jamhuri ya Ireland.
