London, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim ametwaa tuzo ya kocha bora wa mwezi Oktoba kwa Ligi Kuu England (EPL), tuzo ambayo ameibeba kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na timu hiyo Novemba mwaka jana.
Kwa mwezi Oktoba, Amorim ameiwezesha timu hiyo kushinda mechi tatu na hivyo kujipunguzia presha zilizokuwa zikimkabili baada ya kuanza vibaya mechi zake za msimu huu wa 2025-26.
Man United iliuanza mwezi Oktoba kwa ushindi dhidi ya Sunderland kabla ya kupata ushindi ulioshtua wengi dhidi ya mabingwa watetezi wa EPL Liverpool na kumalizia na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Brighton.
Akizungumzia tuzo hiyo Amorim alisema anayetakiwa kupongezwa si yeye bali ni wachezaji waliopata mafanikio baada ya hofu iliYoibuka mwezi Agosti timu hiyo ilipotolewa kwenye Kombe la Carabao na timu ya daraja la chini ya Grimsby Town.
“Wachezaji hakika walifanya vizuri na lengo letu ni kushinda mechi inayokuja kwa sababu hiyo maana yake ni kwamba tunashinda mechi za soka na hilo ndilo lengo letu,” alisema Amorim.
Hii pia inakuwa mara ya kwanza kwa kocha wa Man United kutwaa tuzo hiyo tangu Erik ten Hag afanye hivyo mara ya mwisho Novemba 2023.
Katika mechi ya mwisho ya Man United ya EPL iliyochezwa Jumamosi iliyopita, timu hiyo ilitoka sare na Nottingham Forest na kwa sasa inashika nafasi ya nane kwenye ligi hiyo.
Naye mshambuliaji wa Man United, Bryan Mbeumo ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Oktoba baada ya kufunga mabao matatu katika kipindi hicho kutoa asisti katika mechi za ushindi za timu hiyo.
