Madrid, Hispania
Klabu ya Real Madrid inadaiwa imetoa ruhusa kwa mshambuliaji wake Vinicius Junior kuondoka katika timu hiyo baada ya tafrani iliyoibuka katika mechi na mahasimu wao Barcelona maarufu Clasico.
Vyanzo mbalimbali vya habari leo Jumatano, Novemba 5, 2025 vimedai kuwa uamuzi huo umefikiwa huku habari zaidi zikidai kuwa Vinicius mwenye umri wa miaka 25 huenda akaondoka wakati wa dirisha dogo la usajili la mwezi Januari.
Vinicius Jr ambaye pia ni mshambuliaji tegemeo wa timu ya taifa ya Brazil, ni wazi klabu kadhaa Ulaya zitakuwa tayari kufika bei mara Real Madrid watakapotangaza rasmi taarifa za kumuuza mchezaji huyo.
Katika mechi ya Clasico iliyopigwa hivi karibuni na Real Madrid kutoka na ushindi wa mabao 2-1, Vinicius Jr alitolewa dakika ya 72 jambo lililomkera na kuonesha hasira za wazi dhidi ya kocha wake, Xabi Alonso.
Baada ya kutolewa na kuonesha kutoridhishwa na maamuzi ya Alonso, Vinicius Jr alikwenda moja kwa moja kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ingawa baadaye alirejea kwenye benchi na kuungana na wachezaji wenzake.
Baadaye Vinicius Jr aliingia katika vurugu na wachezaji wa Barca huku akionekana kumlenga zaidi Lamine Yamal na kumtolea kauli za dhihaka ikiwamo kudai kuwa anaongea sana lakini alichofanya uwanjani ni kutoa pasi za visigino.
Katika vurugu baina ya wachezaji wa timu hizo mbili ikiwamo kushikana na kusukumana, wachezaji watano walipewa kadi za njano na mmoja Andriy Lunin wa Real Madrid, alipewa kadi nyekundu.
Akizungumza baada ya mechi Alonso alionekana kupuuza hasira za Vinicius Jr za kutolewa na badala yake alisema kwamba alikuwa makini zaidi katika mambo mazuri yakiwamo mazuri ya Vinicius Jr na hayo mengine yangezungumzwa baadaye.
Kuhusu vurugu baina ya wachezaji wa timu hizo mbili, Alonso alisema hakuna sababu ya kuweka mkazo katika jambo hilo kwani ni tukio la mara moja na linalopita na katika soka mambo hayo hutokea.
Kimataifa Vinicius ruksa kuondoka Madrid
Vinicius ruksa kuondoka Madrid
Read also
