Manchester, England
Mshambuliaji nyota wa Man City, Erling Haaland amepuuza kitendo cha kulinganishwa na mastaa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wanaotamba katika rekodi za mabao akisema hakuna wa kusogelea rekodi za mabao za wachezaji hao.
Haaland mwenye umri wa miaka 26, amefunga mabao 26 katika mashindano yote kwa Man City na timu yake ya taifa ya Norway katika kipindi cha karibuni hivyo kufikisha jumla ya mabao 327 katika soka la ushindani hadi sasa.
Mchezaji huyo pamoja na rekodi hiyo ya kuvutia bado ameachwa mbali na wakongwe, Messi mwenye miaka 38 akiwa hadi sasa na jumla ya mabao 892 na Ronaldo mwenye miaka 40 akiwa na mabao 952 huku malengo yake yakiwa kufikisha mabao 1000.
Alipoulizwa kama anajiona kuwa karibu na mastaa hao, Haaland alikataa kulinganishwa na Messi na Ronaldo na kufafanua kuwa hakuna ambaye ataweza kuwasogelea wawili hao katika rekodi ya kufunga mabao.
Haaland alijiunga na Man City msimu wa 2022-23 akitokea Borussia Dortmund na katika msimu huo wa kwanza alifunga mabao 56, idadi ambayo hadi sasa ndiyo kubwa zaidi kwa mchezaji huyo kwa msimu mmoja.
Alipoulizwa kuhusu rekodi hiyo kama ana mpango wa kuivunja msimu huu, Haaland alisema kwa sasa anajiona yuko katika mazingira mazuri lakini suala la rekodi wala halipo katika fikra zake ikiwamo rekodi ya mabao katika Ligi Kuu England iliyowekwa na Alan Shearer.
“Kufikiria rekodi ninazoweza kuzivunja hilo ni jambo la mwisho katika fikra zangu, ninachofanya kwa sasa ni kuisaidia timu ishinde mechi zake, hiyo ndiyo kazi yangu na ndilo ninalolifikiria,” alisema Haaland.
