Liverpool, England
Nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk amesema shutuma zilizotolewa na mshambuliaji wa zamani wa England, Wayne Rooney akilaumu kukosekana uongozi katika Liverpool, ni shutuma zenye ugoigoi.
Rooney ambaye pia alikuwa mshambuliaji wa Man United kabla ya kugeukia kazi ya ukocha na sasa uchambuzi wa soka, katika hoja yake alihusisha tatizo la kiuongozi katika Liverpool na kiwango kibovu cha timu uwanjani.
Liverpool ambao msimu uliopita walibeba taji la Ligi Kuu England (EPL) wakati kocha wao Arne Slot akiwa katika msimu wake wa kwanza, mambo yamekuwa mabaya kwao msimu huu kwa kutopata matokeo mazuri.
Mwenendo huo wa Liverpool ndio uliomuibua Rooney ambaye pia amewalaumu wachezaji Van Dijk na Mohamed Salah akidai kwamba hawajaiongoza vyema timu hiyo katika msimu huu ingawa mambo ya timu hiyo yalianza kunyooka Jumamosi iliyopita.
Akimjibu Rooney, Van Dijk alisema kwamba hakumsikia Rooney kusema lolote msimu uliopita ambao walibeba taji na hata anachokisema mshambuliaji huyo wa zamani hakimuumizi chochote.
“Hainuimizi mimi, ni kauli ya mchezaji mkongwe, mkubwa na aliyewavutia wengi, ninachoweza kusema ni mambo mazuri kumhusu yeye (Rooney) lakini alichokisema naweza kusema ni shutuma zenye ugoigoi,” alisema Van Dijk.
Kwa upande wake Rooney alisema anashikilia msimamo wa maoni yake kuhusu Liverpool ingawa alimsifu Van Dijk akisema kwamba amekuwa mmoja wa mabeki bora duniani kwa miaka mitano iliyopita.
“Namheshimu, Virgil, nafikiri ni mchezaji mzuri, ila kwa sasa kazi yangu nikiwa mchambuzi wa soka ni kutoa maoni yangu kwa kile ninachokiona,” alisema.
Rooney pia alisema ana uhakika kama ataulizwa mchezaji huyo au kocha Arne Slot atakiri kwamba hajawa mzuri kama alivyokuwa miaka michache iliyopita na kwa maana hiyo ndio maana yeye (Rooney) anasimamia maoni aliyoyatoa.
