Munich, Ujerumani
Klabu ya Bayern Munich imesema beki wa zamani wa timu hiyo na timu ya taifa ya Ujerumani, Jerome Boateng (pichani juu) hatokuwa tena akienda katika klabu hiyo kwa ajili ya kujiendeleza katika kazi ya ukocha.
Uamuzi huo umetokana na kitendo cha baadhi ya mashabiki wa timu hiyo hivi karibuni kumpinga mchezaji huyo kwa mabango uwanjani baada ya kukutwa na hatia ya kumdhuru mpenzi wake wa zamani.
Kocha wa Bayern, Vincent Kompany ambaye aliwahi kucheza timu moja na Boateng, alinukuliwa mwezi Septemba mwaka huu akisema anamkaribisha Boateng katika timu hiyo ili kuanza mazoezi ya kazi ya ukocha.
Mwaka jana mahakama moja ya mjini Munich ilimpa Boateng (pichani chini alivyo sasa) kifungo cha nje na onyo kwa kosa la kumpiga mpenzi wake wa zamani ingawa Boateng kwa wakati wote amekuwa akikana kufanya kosa hilo.
“Katika makubaliano baina ya klabu ya Bayern na Boateng imekubaliwa kuwa Joreme Boateng hatokuwa akifika kushuhudia mazoezi ya timu ya soka ya Bayern,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.

Taarifa hiyo pia ilimtaja Boateng kuwa ni mtu anayejiona anamahusiano na klabu ya soka ya Bayern na hataki klabu hiyo iingie katika misukosuko kutokana na mjadala wenye utata unaomhusu yeye.
Katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii, Boateng aliiambia klabu hiyo na kocha Kompany kuwa baada ya mazungumzo ya pande mbili kuhusu mjadala ulioibuka dhidi yake ameamua kubadili muelekeo ili kuhakikisha klabu hiyo inajikita katika ubora wa kiwango chake uwanjani.
Boateng amebeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili na Bayern na Kombe la Dunia mwaka 2014 na timu ya taifa ya Ujerumani, alistaafu soka mwezi Septemba mwaka huu, hiyo ni baada ya kuachana na klabu ya LASK Linz ya Austria mwezi mmoja kabla.
