Liverpool, England
Mshambuliaji wa zamani wa Man United na timu ya taifa ya England, Wayne Rooney amehusisha uongozi na matokeo mabaya yanayoikuta Liverpool katika Ligi Kuu England (EPL).
Sambamba na hilo, Rooney pia amesema kwamba kiwango cha mshambuliaji nyota na tegemeo wa timu hiyo, Mohamed Salah ni jambo linalotia hofu.
Jumamosi iliyopita Liverpool ililala kwa mabao 3-2 mbele ya Brentford katika EPL wakati siku inayofuata vinara wa ligi hiyo, Arsenal walitoka na ushindi dhidi ya Crystal Palace na hivyo kuzidi kujiimarisha kileleni mwa ligi hiyo.
Mwenendo wa Liverpool umeibua hofu kwa mabingwa hao watetezi kama wataweza kulitetea taji la ligi hiyo huku Rooney akihoji kama timu hiyo ina viongozi wanaofaa kuipandisha kileleni.
Rooney alisema kwamba ingawa Virgil van Dijk na Mohamed Salah wamesaini mikataba mipya lakini hadhani kama wemeiongoza vyema timu hiyo kwa msimu huu.
“Kwa kuwaangalia tu (Salah na Van Dijk) unaweza kuona mambo mengi na nadhani kwa mtazamo tu tunaona hali tofauti kwa wawili hao, ni wachezaji wawili wa hadhi ya juu katika timu lakini kama kimtazamo hawako sawa hiyo inamuathiri kila mmoja,” alisema Rooney.
Rooney aliongeza kuwa anaweza asiwe sahihi katika hilo lakini kama angekuwa kocha au shabiki wa Liverpool hilo kwake lingekuwa jambo kubwa la kuliangalia.
Alisema Liverpool inahaha kurudi katika kuwa timu ya kushinda baada ya mfululizo wa kiwango kibaya na hawakutegemea kukutana na walichokutana nacho hivyo huu ni wakati wa kocha na viongozi wa timu kufanya tathmini ya haraka.
