Na mwandishi wetu
Timu ya Yanga hatimaye imefuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiichapa Silver Strikers ya Malawi mabao 2-0 na hivyo kufuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 baada ya kulala kwa bao 1-0 katika mechi ya awali.
Yanga iliyokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam leo Jumamosi Oktoba 25, 2025 mbele ya maelfu ya mashabiki wake walioingia bure uwanjani, ilihofiwa kwamba ingeweza kutolewa kutokana na matokeo ya mechi hiyo ya awali.
Alikuwa ni beki Dickson Job aliyeibua upya matumaini ya timu hiyo kusonga mbele mapema dakika ya sita baada ya kuipatia Yanga bao la kwanza baada ya kuuwahi mpira wa kona uliopigwa na Mohamed Doumbia.
Baada ya bao hilo, Yanga waliongeza kasi ya kusaka bao la pili huku wakitawala vyema eneo la kiungo, juhudi ambazo zilizaa matunda dakika ya 34 kwa bao lililofungwa na Pacome Zouzoua kwa pasi ya Maxi Nzengeli.
Ushindi huo unakuwa umeibua matumaini mapya na kurejesha amani kwa viongozi wa Yanga ambao katika siku za karibuni wamekuwa wakisakamwa na mashabiki wao wakidai kutoridhishwa na kiwango cha uchezaji cha timu hiyo.
Uongozi hatimaye ulifikia hatua ya kumtimua kazi kocha mkuu Romain Folz na majukumu yake kukabidhwia wasaidizi wake ambao wataendelea na jukumu hilo kabla ya kocha mpya kuanza kazi.
Wakati huo huo timu ya Singida Big Stars nayo imefuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuibuka na ushndi wa mabao 3-1 dhidi ya Flambeau du Centre FC ya Burundi, mechi iliyopigwa leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo timu hiyo inakuwa imesonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-2 baada ya sare ya bao 1-1 katika mechi ya awali ambayo Singida BS walikuwa ugenini.
Ushindi wa Singida BS unazifanya timu za Tanzania zilizofuzu hatua ya makundi kwenye mashindano ambayo yanaandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kufikia tatu baada ya Yanga na Azam FC na kama Simba itafuzu kesho Jumapili, timu hizo zitakuwa nne.
Kimataifa Yanga yafuzu makundi Ligi ya Mabingwa
Yanga yafuzu makundi Ligi ya Mabingwa
Read also
