Na mwandishi wetu
Azam FC imetinga kwa kishindo hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika ikiichakaza KMKM mabao 7-0 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 9-0 baada ya ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata katika mchezo wa awali.
Ikiwa nyumbani kwenye dimba la Azam Complex Jumamosi hii Oktoba 24, Azam ilianza kuhesabu bao la kwanza dakika ya 22 kwa bao la Idd Nado alipoinasa pasi ya Feisal Salum au Fei Toto.
Dakika nne baada ya bao hilo, Azam waliongeza bao la pili safari hii Nado kwa mara nyingine alihusika kwa kupiga krosi ambayo Jephte Kitambala aliitumia vyema kuipatia Azam bao hilo.
Dakika ya 29, Kitambala aliipatia Azam bao la tatu safari hii kwa pasi ya Fei Toto kabla ya kukamilisha bao la nne, mabao ambayo yalidumu kwa dakika zote 45 za kipindi cha kwanza.
KMKM ilikianza kipindi cha pili kivingine ikifanya mabadiliko ya baadhi ya wachezaji lakini mabadiliko hayo hayakuweza kuwazuia Azam kuendelea na kasi yao ya kusaka mabao.
Kasi hiyo ilizaa mabao ya Abdul Sopu aliyefunga mawili pamoja na Paschal Msindo aliyekamilisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la saba na la mwisho.
Kwa ushindi huo Azam sasa wanaisubiri kwa hamu Novemba 3 ya mwaka huu, siku ambayo droo ya kupanga makundi ya timu zilizofuzu hatua hiyo itakapofanyika na timu hiyo kuwajua wapinzani wake.
Kimataifa Azam yaipa KMKM dozi ya 7-0
Azam yaipa KMKM dozi ya 7-0
Read also
