Na mwandishi wetu
Mambo si mambo kwa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulala kwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Silver Strikers ya Malawi, mechi iliyochezwa Jumamosi hii Oktoba 18, 2025 kwenye Uwanja wa Taifa wa Bingu nchini Malawi.
Matokeo hayo yanaiweka Yanga pagumu kwani sasa itakuwa na kazi ya kupindua matokeo ikiwa nyumbani katika mechi ya marudiano inayotarajia kuchezwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ili kufufua matumaini ya kuendelea na michuano hiyo.
Bao pekee la Silver Strikers lilipatikana dakika ya 76 mfungaji akiwa ni Adulu baada ya timu hiyo kufanya shambulizi la kushtukiza na Yanga kushindwa kukabiliana nalo.
Yanga ikiwatumia nyota wake Pacome Zouzoua na wengineo walishindwa kuzitumia dakika 14 za mwisho kupata bao la kusawazisha na kuongeza la pili kwani hadi mwisho wa mchezo matokeo yalibaki kuwa mazuri kwa wenyeji Silver.
Matokeo yoyote ya sare au kufungwa kwenye mechi ya marudiano yataifanya Yanga kupata aibu kwa kuaga mapema michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika bila kugusa hatua ya makundi.
Kwa kipindi kirefu mashabiki wa Yanga wamekuwa wakimlalamikia kocha wao Romain Folz kwa madai kuwa ameshindwa kuifanya timu yao icheze vizuri na bila shaka matokeo ya mechi na Silver yanazidi kumuweka pagumu kocha huyo.
Kimataifa Ugenini pagumu kwa Yanga
Ugenini pagumu kwa Yanga
Read also
