Munich, Ujerumani
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane amesema yuko tayari kwa ajili ya mazungumzo ya kusaini mkataba mpya na klabu hiyo huku akiupotezea mpango wa kurudi kwenye Ligi Kuu England (EPL).
Kane kwa sasa ni kama tayari ametumikia nusu ya mkataba wake wa miaka minne na Bayern, mkataba ambao alisaini majira ya kiangazi mwaka 2023 kwa thamani ya Euro 86.3 milioni akitokea Tottenham Hotspur.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32 tayari ameifungia Bayern mabao 103 katika mechi 106 na kuisaidia timu hiyo kubeba taji la Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga ambalo ni taji lake la kwanza.
Kauli ya Kane imekuja ikiwa ni siku chache zimepita baada ya kocha wa Tottenham, Thomas Frank kunukuliwa akisema kwamba angependa kumuona Kane akirudi kucheza EPL ambapo anahitaji mabao 48 katika ligi hiyo ili kuipiku rekodi ya muda wote ya mabao 260 inayoshikilia na Allan Shearer.
Kane ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya England amesema kwamba kwa sasa hana tena nia ya kurudi nyumbani England kama ilivyowahi kuwa hapo kabla na badala yake anachofikiria ni kuongeza mkataba Bayern.
“Kuhusu suala la kuendelea kubaki hapa muda mrefu zaidi, hilo naliona, nilizungumza wazi wiki chache zilizopita na ingawa bado sijafanya mazungumzo na Bayern lakini ikitokea hivyo nitakuwa tayari kwa mazungumzo nao mazuri tu,” alisema Kane.
Kane aliyetamba na kujipatia umaarufu England wakati akiichezea Tottenham, hata hivyo alitahadharisha kwamba mambo yote hayo pia yatategemea hali itakavyokuwa mwaka ujao na nini watakachokifanikisha pamoja lakini kwa sasa anachoweza kusema ni kwamba wapo katika hatua nzuri na hana jambo jingine analofikiria.
Aliongeza kwa kusema kwamba akiulizwa kuhusu EPL hana anachojua lakini kama angeulizwa siku ile anaondoka England na kuhamia Bayern angesema yuko tayari kurudi England lakini kwa sasa suala la kurudi England limepungua ingawa hawezi kusema kamwe hatorudi England.
