Na mwansishi wetu
Kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Septemba baada ya kufanya vizuri kwenye michezo miwili ya Yanga ya Ligi Kuu NBC msimu huu wa 2025-26.
Taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) iliyopatikana leo Jumapili, Oktoba 5, 2025 imeeleza kuwa kamati ya tuzo hizo ya TFF imeeleza kuwa kipa huyo ameonesha kiwango kizuri na chenye mwendelezo.
Hadi kuibuka kinara wa tuzo hiyo, Diarra amewashinda Anthony Tra-Bi wa Singida Black Stars (Singida BS) na Mohamed Bakar wa JKT Tanzania alioingia nao fainali katika mchakato huo.
Diarra alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo miwili ya ligi ambayo timu yake ilicheza dhidi ya Pamba Jiji na kuibuka na ushindi wa nyumbani wa mabao 3-0.
Katika mechi ya pili, Yanga ikiwa ugenini dhidi ya Mbeya City walitoka sare ya 0-0 na hivyo Diarra kutoruhusu timu yake kufungwa hata bao moja.
Kwa upande wa kocha bora wa mwezi Septemba tuzo hiyo imekwenda kwa Ahmad Ally wa JKT Tanzania ambaye katika mchakato wa kuwania tuzo hiyo aliingia fainali na Romain Folz wa Yanga na Miguel Gamondi wa Singida BS.
Kilichombeba kocha huyo wa JKT ni mechi ya ugenini dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika ambayo walitoka sare ya 0-0 na baadaye mechi nyingine ya ugenini dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga ambayo JKT walishinda kwa mabao 2-1.
Soka Diarra mchezaji bora Septemba
Diarra mchezaji bora Septemba
Read also
