Barcelona, Hispania
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick amesema haiwezekani kusema kama mshambuliaji wake Lamine Yamal atakuwa fiti kwa ajili ya mechi na mahasimu wao Real Madrid maarufu Clasico baadaye mwezi huu.
Yamal, 18, aliyekuwa akiandamwa na matatizo ya misuli, alirejea uwanjani kwa mara ya kwanza akiingia kipindi cha pili katika mechi ya ushindi dhidi ya Real Sociedad na Jumatano iliyopita alicheza dakika zote 90 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG ambayo Barca walipoteza.
Baada ya mechi na PSG ilielezwa kuwa Yamal hakuwa vizuri licha ya kucheza dakika zote 90 na inadaiwa kwamba anatarajia kuikosa mechi ya leo Jumapili Oktoba 5, 2025 dhidi ya Sevilla.
Sambamba na hilo, Yamal pia atazikosa mechi za kimataifa na timu ya taifa ya Hispania na Flick akaongeza kuwa huenda mchezaji huyo pia akaikosa mechi yao na Real Madrid itakayopigwa Oktoba 26 mwaka huu kwenye dimba la Santiago Bernabéu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuulizwa kuhusu hali ya Yamal, kocha Flick alisema amezungumza na mchezaji huyo na hali yake si mbaya sana lakini kiujumla haijawa nzuri.
“Hii ndio hali ya Lamine, kwa majeraha yake si rahisi kujua lini hasa atarudi uwanjani, si rahisi kusema sasa yuko sawa anaweza kucheza katika kipindi cha wiki mbili, tatu au nne au atacheza kwenye Clasico, hilo haliwezekani,” alisema Flick.
Flick alisema kwamba ni lazima kusubiri kwa kuwa wakati huu anafanya mazoezi na timu ya wataalamu ili kuangalia hali yake hatua kwa hatua ili kuwa na uhakika wa maendeleo ya majeraha yake kiujumla.
Yamal alipata matatizo ya misuli Septemba mwaka huu wakati akiiwakilisha Hispania na hivyo kukosa mechi nne za Barca ambapo Flick aliwalaumu mabosi wa timu ya taifa ya Hispania kwa kutomuangalia vizuri mchezaji huyo.
