Na mwandishi wetu
Wakati mashabiki Simba wakisubiri kwa hamu kumjua kocha mpya wa timu hiyo, klabu hiyo imemtambulisha Dimitar Pantev kuwa meneja mkuu tofauti na matarajio kwamba angepewa nafasi ya kocha mkuu iliyokuwa ikishikiliwa Fadlu Davids.
Simba imekuwa ikinolewa na kocha msaidizi Suleiman Matola na Hemed Suleiman ‘Morocco’ ambaye anaiongoza kwenye mechi za kimataifa na imekuwa ikisaka kocha wa kudumu tangu kuondoka kwa Fadlu aliyejiunga na Raja Casablanca ya Morocco.
Katika mchakato wa kumsaka mrithi wa Fadlu jina la Pantev, raia wa Bulgaria limekuwa likitajwa zaidi lakini tofauti na matarajio ya mashabiki wengi, taarifa ya uongozi wa Simba iliyopatikana Ijumaa, Oktoba 3, 2025 imemtangaza Pantev kuwa meneja mkuu na si kocha mkuu.
Uamuzi huo wa uongozi wa Simba umeibua mjadala miongoni mwa mashabiki hasa kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi wakidai kwamba klabu hiyo imevutiwa na ubora wa kocha huyo lakini hana sifa stahiki na ndio maana wakaamua kumpa nafasi ya umeneja lakini kimsingi atakuwa akifanya kazi ya Fadlu.
Wengine wanadai kuwa Simba imekuja kisasa zaidi kwa kuwa na meneja mkuu katika timu badala ya kocha kama ambavyo baadhi ya klabu barani Ulaya zimekuwa zikifanya kwa kumpa majukumu ya timu meneja mkuu.
Pantev 49, kabla ya Gaborone United amewahi kufanya kazi ya ukocha kwao Bulgaria na baadaye barani Asia na kwa Afrika alianzia Cameroon kabla ya kuhamia Botswana Januari mwaka huu alipojiunga na Gaborone United na kuiwezesha kubeba taji la Ligi Kuu Botswana.
Soka Kocha mpya Simba azua mjadala
Kocha mpya Simba azua mjadala
Read also
