Na mwandishi wetu
Yanga imeanza kuona ugumu wa Ligi Kuu NBC baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na Mbeya City katika mechi iliyochezwa leo Jumanne, Septemba 30, 2025 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya huku mashabiki wa timu hiyo wakimlaumu kocha wao, Romain Folz.
Mashabiki wamekerwa na matokeo hayo ambayo hawakuyatarajia baada ya timu hiyo kushinda mechi tano zilizopita zikiwamo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika chini ya kocha Folz.
Katika ushindi wa mechi zilizopita wapo baadhi ya mashabiki waliotilia shaka uwezo wa timu yao na kuhoji kama kocha Folz ataweza kuifikisha timu hiyo mbali na wengine wakishauri Yanga kuachana na kocha huyo.
Kelele za mashabiki dhidi ya kocha huyo zilianza kusikika mwanjani hapo mara baada ya mwamuzi kumaliza mechi hiyo iliyokuwa kali na yenye ushindani kwa pande zote.
Yanga iliuanza mchezo kwa kasi na kuonesha kila dalili za kusaka bao la mapema hasa katika dakika sita za mwanzo lakini safu ya ulinzi ya Mbeya City ikiongozwa na kipa Beno Kakolanya ilikuwa imara.
Wakionekana kama walikuwa wakiisoma Yanga, Mbeya City nao walianza kuonesha makali yao kwa kulishambulia lango la Yanga na kuufanya mchezo uchangamke kwa timu hizo kushambuliana mara kwa mara.
Kipindi cha pili timu ziliendelea kuonesha ubora, Pacome Zouzoau wa Yanga aliisumbua safu ya ulinzi ya Mbeya City wakati beki wa Mbeya City, Ibrahim Ame naye mara kadhaa alionesha ubora katika kudhibiti mashambulizi ya wachezaji wa Yanga.
Baada ya mechi hiyo, kocha Folz alisema kwamba hakutarajia matokeo hayo na kuahidi kwenda kuboresha kikosi chake akikiri kwamba yapo makosa ambayo wanakwenda kuyafanyia kazi.
Kimataifa Yanga, Mbeya hakuna mbabe, kocha alaumiwa
Yanga, Mbeya hakuna mbabe, kocha alaumiwa
Read also
