Manchester, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim amesema kwamba hana hofu yoyote kuhusu kibarua chake licha ya mambo kuonekana yakienda kombo na hivyo kuacha maswali kuhusu hatma yake katika timu hiyo.
Amorim ambaye hivi karibuni aliibua matumaini baada ya kupata ushindi dhidi ya Chelsea lakini leo Jumamosi hali imekuwa tete baada ya timu yake kulala kwa mabao 3-1 mbele ya BrenTford katika mechi nyingine ya Ligi Kuu England (EPL).
Baada ya kumaliza nafasi ya 15 katika msimu uliopita wa EPL, kulikuwa na ahadi na matumaini makubwa ya kufanya vizuri msimu huu lakini hali imekuwa tofauti huku majaliwa ya kocha Amorim katika timu hiyo yakionekana kuwa njia panda.
Amorim hata hivyo pamoja na mazingira kuonekana magumu kwa upande wake bado na kazi yake kugeuka mjadala, bado mwenyewe amesisitiza kwamba hana hofu yoyote ya kupoteza kazi na yeye si mtu wa aina hiyo.
“Sijawahi kuwa na wasiwasi wa kupoteza kazi, mimi si mtu wa aina hiyo na uamuzi wa jambo hilo haunihusu mimi, nitafanya kila kitu katika ubora kwa kila dakika ambayo nitakuwa hapa,” alisema Amorim.
Vigogo wa Man United wamewahi zaidi ya mara moja kuelezea walivyo na imani na kocha huyo na wanavyomuunga mkono lakini kwa mazingira ya sasa ni dhahiri kwamba imani hiyo inazidi kuacha maswali.
Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa huu ni wakati sahihi kwa kocha huyo kubadili mfumo wa uchezaji badala ya kushikilia staili yake ya 3-4-2-1 ambao unaonekana kutompa mafanikio yaliyotarajiwa.
