London, England
Arsenal huenda ikamkosa mshambuliaji wake, Noni Madueke kwa kipindi cha wiki sita hadi nane kutokana na majeraha ya goti aliyoyapata katika mechi ya juzi Jumapili dhidi ya Man City iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.
Madueke, 23 ambaye amejiunga na Arsenal akitokea Chelsea katika majira ya kiangazi, alilazimika kutolewa wakati wa mapumziko na amekuwa akifanyiwa vipimo kujua ukubwa wa tatizo lililomkuta.
Habari za ndani zinadai kwamba upo uwezekano mkubwa kwa mchezaji huyo kukosa mechi za Arsenal kwa wiki sita hadi nane ingawa taarifa rasmi bado hazijatolewa.
Habari hizo zinakuwa pigo kubwa kwa kocha wa Arsenal Mikel Arteta na kocha wa England, Thomas Tuchel baada ya mchezaji huyo kuanza vizuri msimu huu na kuibua matumaini makubwa kwa makocha hao.
Ikitokea Madueke kuwa nje kwa kipindi cha wiki nane maana yake ni kwamba atakuwa nje ya uwanja hadi mwezi Novemba na hivyo kumfanya akose baadhi ya mechi muhimu za Arsenal za Ligi ya Mabingwa Ulaya na zile za Ligi Kuu England.
Kwa upande wa England mshambuliaji huyo huenda akazikosa mechi zijazo dhidi ya Wales na Latvia hapo hapo kukiwa na wasi wasi kama atakuwa tayari kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Serbia na Albania zitakazochezwa katikati ya mwezi Novemba.
Arsenal itaumana na Sunderland Novemba 8 katika mechi ya Ligi Kuu England na kama ataikosa mechi hiyo basi mashabiki wa timu hiyo wamtarajie mchezaji huyo katika mechi ya London Derby dhidi ya Tottenham ambayo itachezwa Novemba 23.
Kimataifa Madueke nje wiki nane
Madueke nje wiki nane
Read also
