Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Simba imemtangaza kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kuwa kocha wao wa muda akichukua nafasi ya Fadlu Davids aliyeachana na timu hiyo.
Taarifa ya klabu ya Simba imeeleza kuwa kocha Morocco ambaye tayari ameanza majukumu hayo mapya, ataiongoza timu hiyo kwenye mechi za kimataifa kwa kuwa kocha wao msaidizi, Suleiman Matola ana kadi nyekundu.
Uongozi wa Simba katika taarifa yao walilishuruku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kumruhusu Morocco kuiongoza timu hiyo licha ya kuwa na majukumu mengine kwenye timu ya taifa.
Simba wamefafanua kuwa Morocco ataifanya kazi hiyo wakati huu klabu hiyo ikiendelea na mchakato wa kumsaka kocha mpya wa kudumu ambaye atakabidhiwa timu.
Kwa mantiki hiyo, Morocco ataanza kuliongoza benchi la timu hiyo kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United, mechi ambayo itachezwa Septemba 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Katika mechi ya kwanza ambayo Simba ilikuwa ugenini Botswana, timu hiyo ilitoka na ushindi wa bao 1-0 na hiyo ilikuwa mechi ya mwisho kwa Fadlu kuingoza Simba.
Fadlu, kocha kutoka Afrika Kusini ameachana na Simba baada ya kuitumikia kwa mwaka mmoja na kuiwezesha kufikia hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu NBC.
Kimataifa Morocco apewa majukumu Simba
Morocco apewa majukumu Simba
Read also
