Na mwandishi wetu
Baada ya uvumi wa hivi karibuni, hatimaye uongozi wa Simba umetangaza rasmi kuachana na kocha Fadlu Davids hapo hapo zikiibuka habari kwamba klabu ya Raja Casablanca ya Morocco imemtangaza kuwa kocha wao mpya.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwapo habari kwamba kocha huyo alikuwa katika mazungumzo akitaka kuachana na Simba huku zikitajwa sababu mbalimbali ikiwamo kutopata ushirikiano aliohitaji kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo.
Simba katika taarifa yao iliyopatikana leo Jumatatu, Septemba 22, 2025 ilieleza kuwa uongozi wa klabu hiyo na kocha huyo kutoka Afrika Kusini wamefikia makubaliano ya kuvunja mkataba baada ya kufanya naye kazi kwa takriban mwaka mmoja.
Taarifa hiyo pia imefafanua kuwa makubaliano hayo ya kuvunja mkataba yametokana na matakwa binafsi ya kocha huyo kwa uongozi wa Simba ingawa haikufafanuliwa kwa mapana kuhusu matakwa hayo.
Uongozi wa Simba hata hivyo ulimshukuru Fadlu kwa kuiwezesha timu yao kufikia hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na kumaliza Ligi Kuu NBC nafasi ya pili, yote hayo akiyafanikisha katika msimu wa 2024-25.
Fadlu anaondoka akiwa ndio kwanza ameanza kuiongoza Simba katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika juzi Jumamosi na kuibuka na ushindi wa ugenini wa bao 1-0 dhidi ya Gaborone United ya Botswana, alitarajiwa kuendeleza mafanikio hayo kwa msimu huu mpya wa 2025-26 ambao ndio kwanza umeanza.
Katika taarifa hiyo uongozi wa Simba haukueleza lolote kuhusu kocha atakayechukua nafasi ya Fadlu ingawa jina la kocha wa zamani wa Yanga, Nasredinne Nabi limekuwa likitajwa zaidi hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Taarifa nyingine zilizopatikana jioni hii mara baada ya Simba kutoa taarifa yao zinadai kuwa klabu ya Raja Casablanca imemtangaza Fadlu kuwa kocha mkuu akichukua nafasi ya Lassaad Chabbi kutoka Tunisia.
Habari hizo zinadai kuwa Raja wameamua kusitisha mkataba na Chabbi baada ya makubaliano ya pande mbili baada ya kufanyika kwa tathmini ya timu hiyo katika kipindi cha maandalizi ya msimu mpya wa 2025-26.
Fadlu si jina geni katika klabu ya Raja, aliwahi kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo katika msimu wa 2024-25 na anatajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa kwenye mafanikio ya timu hiyo iliyomaliza msimu huo na mataji mawili bila kupoteza hata mechi moja.
Kimataifa Fadlu aondoka Simba, atambulishwa Raja
Fadlu aondoka Simba, atambulishwa Raja
Read also
