Barcelona, Hispania
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick amewalaumu mabosi wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya Hispania kwa kutomjali Lamine Yamal baada ya mchezaji huyo kuumia akiwa kwenye mechi za kimataifa.
Yamal ambaye katikati ya wiki alikuwa na timu ya taifa ya Hispania kwenye mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026, kutokana na kuumia huko sasa ataikosa mechi ya Jumapili hii ya La Liga dhidi ya Valencia.
Flick alisema Yamal ameichezea Hispania mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Bulgaria na Uturuki licha ya kuwa na majeraha ya misuli lakini benchi la ufundi la Hispania chini ya kocha Luis de la Fuente hawakujali hilo.
Yamal mwenye umri wa miaka 18, mbali na kukosa mechi na Valencia huenda Alhamisi ijayo pia akashindwa kuiwakilisha Barca kwenye mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Newcastle United.
Akifafanua Flick alisema Yamal alikwenda timu ya taifa akiwa na maumivu na hakufanya mazoezi badala yake akapewa dawa za kuondoa maumivu ili acheze, alicheza dakika 79 mechi ya kwanza na ya pili dakika 73 na mechi zote Hispania walikuwa mbele kwa mabao matatu.
“Hakufanya mazoezi baada ya mechi ya kwanza, huku si kujali afya ya wachezaji, Hispania wana timu bora duniani, katika kila eneo wapo katika ubora kwa namna ya kipekee, kwa kweli mazingira haya (ya Yamal) yamenisikitisha,” alisema Flick.
Yamal ameuanza msimu huu wa 2025-26 akiwa katika kiwango kizuri, tayari ametoa asisti mbili na kuifungia Barca mabao mawili katika mechi tatu za awali za La Liga na baada ya hapo akatoa asisti mbili kwenye timu yake ya taifa.
Flick hata hivyo alisema hajazungumza lolote na kocha wa Hispania kwa alichodai kuwa huenda Kihispania chake (Flick) si kizuri au Kiingereza cha kocha (De La Fuente) si kizuri na hilo kwake analiona kuwa ni tatizo.
Katika mechi dhidi ya Valencia, Barca pia itamkosa kiungo Frenkie de Jong ambaye amepata majeraha wakati akiiwakilisha timu yake ya taifa ya Uholanzi.
